Majaji wapinga uamuzi wa Rais Misri

Raisn Mohamed Morsi

Makabiliano yametokea kati ya mamia ya wafuasi na wapinzani wa Rais Mohammed Morsi.

Mapigano hayo yametokea huku taharuki ikitanda kuhusu kuachishwa kazi kwa mshirika wa karibu wa aliyekuwa Rais Hosni Mubarak.

Rais Mohammed alimwachisha kazi kiongozi wa mashtaka ambaye anatuhumiwa kuhusika na mauaji ya waandamanaji waliokuwa wanashiriki maandamano ya kumng'oa mamlakani Hosni Mubarak mwaka jana.

Chama cha Rais Morsi kiliitisha maandamano katika medani ya Tahrir kutaka Rais Morsi kumfuta kazi mwendesha mashtaka huyo.

Bwana Morsi alijaribu kumfuta kazi siku ya Alhamisi, lakini mwendesha mashtaka huyo akakataa kujiuzulu akisema kuwa Rais Morsi hana mamlaka ya kumfuta kazi.

Kwingineko kikundi kimoja cha majaji nchini Misri, kimemshutumu Rais Mohammed Mursi kwa kujaribu kumfuta kazi kiongozi wa mashtaka kama kichekesho kikubwa.

Kiongozi wa majaji hao alinukuliwa akisema kuwa enzi ya madikteta imepitwa na wakati.

Rais alimfuta kazi Maguid Mahmoud, ingawa amekataa kuacha wadhifa wake.

Hatua hii dhidi ya Mahmoud, ilikuja baada ya watu kughadhabishwa juu ya hatua za serikali kuwaachilia huru wafuasi wa utawala wa Mubarak.

Wafuasi ishirini na wanne wa Mubarak walifutiliwa mashtaka ya kuwashambulia waandamanaji wakati wa mapinduzi ya mwaka jana.

Walituhumiwa kwa kutumia farasi na ngamia kuvunja maandamano ya mwaka 2011 mjini Cairo, na kusababisha vifo vingi.

No comments:

Post a Comment