Milipuko
ya sauti ya juu pamoja na milio ya risasi ilisikika leo mjini Maiduguri,
Kaskazini mwa Nigeria, mji ambao umeshuhudia ghasia na vurugu
zinazosababishwa na kundi haramu la wapiganaji wa kiisilamu la Boko
Haram.
Taarifa kuhusu mashambulizi hayo bado hazijatolewa , lakini inaarifiwa angalau watu kumi wameuawa ikiwemo wanajeshi kadhaa.
Mwalimu wa shule ya msingi aliuawa huku mnara wa kupeperushia matangazo ya redio ukichomwa.
Mapema mwezi huu, walioshuhudia makabiliano kati
ya jeshi na washukiwa wa Boko Haram, walisema kuwa wanajeshi waliwapiga
risasi raia 30 baada ya shambulizi la bomu dhidi ya kambi ya jeshi
mjini Maiduguri.
Katika tukio la hivi karibuni, ripoti zinasema
kuwa wanajeshi walifunga karibu kila barabara mjini wakati mashambulizi
yalipoanza Jumatatu adhuhuri na kuendelea hadi masaa ya usiku.
Walioshuhudia tukio hilo wanasema kuwa mapema
Jumatatu mtu aliyekuwa amejihami alishambulia kwa risasi polisi
aliyekuwa anashika doria mjini humo karibu na kizuizi barabarani.
Mapema mwezi huu, wanajeshi mjini Maiduguri, waliwashambulia watu baada ya kutokea shambuli la bomu na kumuua mwanajeshi mmoja.
Walichoma maduka ya watu pamoja na nyumba.
Jeshi lilikana mauaji hayo ingawa waandishi wa habari wanasema kuwa lilitoa maelezo ya kina kuhusu kilichotokea
Mashambulizi Kaskazni mwa Nigeria ambayo yamefanywa na Boko Haram yamesababisha vifo vya watu 1,400 tangu mwaka 2010.
No comments:
Post a Comment