Mdee Amvaa Lwakatare
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
VIONGOZI AINA YA MCHUNGAJI GETRUDE LWAKATARE NI AIBU KWA
TAIFA
Hivi karibuni Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi Prof. Anna
Tibaijuka na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Terezya
Huvisa walitoa tamko kwamba nyumba zote zilizojengwa kando kando ya fukwe
za bahari na mito zitabomolewa, bila wamiliki kulipwa fidia kutokana na kukiuka
Sheria za Ardhi na Mazingira za mwaka 1992, 1995 na 2004. Kauli hiyo ilitokana
na ukweli kwamba imekuwa ni jambo la kawaida kwa watu wenye nguvu ya
fedha kuharibu mazingira kwa makusudi pasipo kujali athari ambazo zinaweza
kutokea sasa na baadae kwa wakazi wa maeneo husika, jamii inayowazunguka
na taifa kwa ujumla!
Kwa watu wengi, kauli ya mawaziri hao ilionekana kama ni hatua muhimu
sana katika kulinda mazingira ya fukwe zetu na jamii nzima hasa kutokana na
umuhimu wa kulinda mazingira katika wakati huu wa athari za mabadiliko ya
tabianchi. Lakini baadhi yetu tuliona kama ni mwendelezo wa kauli za Serikali
ambazo utekelezaji wake ama huwa ni wa mashaka au ukitekelezwa basi
utekelezaji wake hutawaliwa na upendeleo wa hali ya juu kwa watu wenye fedha
na nafasi kubwa serikalini (vigogo).
Moja kati ya nyumba iliyotakiwa kubomolewa imejengwa kwenye viwanja namba
2019-2020 Kawe Beach, katika fukwe za Bahari ya Hindi. Viwanja ambavyo
vilipatikana kwa ushirikiano wa Mchungaji Lwakatare na tapeli maarufu wa Ardhi
jijini Dar es salaam, anayejulikana kwa jina la Frank Mushi.
Ikumbukwe kwamba katikati ya mwezi Julai, 2012 wananchi waliojenga nyumba
katika maeneo yanayosemekana ni tengefu ya Jangwani Beach, Mto Ndumbwi
na Mto Mbezi walivunjiwa nyumba katika operesheni iliyoendeshwa na Baraza
la Mazingira la Taifa (NEMC). Operesheni ambayo ilihusisha takriban nyumba
15 na kuta ( fences) 8. Katika nyumba hizo, mojawapo iliyotakiwa kuvunjwa ni ya
Mchungaji Getruda Lwakatare. Lakini kwa sababu ambazo wahusika, akiwemo
yeye mwenyewe na serikali, wanazifahamu, nyumba yake haikuguswa!
Wakati wananchi wanaofahamu ukweli wa mambo, wakiwa bado wanahoji
chinichini juu ya upendeleo wa kitabaka ulio wazi, hivi karibuni wameshuhudia
kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari, ikiripotiwa kuwa Mchungaji
Lwakatare (Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God na Mbunge wa Bunge
la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ) amehamia kwenye nyumba yake
mpya. Nyumba ambayo ilipaswa kuwa imebomolewa kwa sababu imejengwa
kwenye viwanja ambavyo ni kinyume cha sheria kujenga katika maeneo hayo.
Kuvunja sheria kwa uwazi namna hii, huku wengine wakichukuliwa hatua kwa
kuvunja sheria hiyo hiyo, si tu ni ’double standards’, bali kunaweza kutafsiriwa ni
kuitia serikali mfukoni.
Kitu kibaya zaidi ni kwamba kiongozi huyo alishataarifiwa tangu mapema juu
ya ubatili wa kujenga katika eneo hilo, kupitia kwa huyo Frank Mushi kabla
hata ujenzi wa nyumba hiyo haujaanza. Ikumbukwe pia kuwa viwanja hivyo
vilipatikana na ujenzi huo kuwezekana baada ya eneo la bahari na mto kujazwa
kifusi na mawe!
Kwa kutambua kuwa kuendelea na ujenzi katika eneo hilo ni kuvunja sheria za
nchi zinazohusu utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya jamii nzima, Mchungaji
Lwakatare aliendelea kwa kujiificha nyuma ya mgongo wa huyo Mushi, akijifanya
hahusiki kabisa na kilichokuwa kikiendelea katika eneo husika.
Uthibitisho wa ubatili wa kujenga katika viwanja husika:
1) Tarehe 4/1/2011 Wizara ya Ardhi kupitia barua yenye Kum. Namba
LD/297571/18 waliandika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Manispaa ya Kinondoni kuhusiana na uvamizi wa kiwanja nana 2019 na
2020 Mbezi Kawe. Barua husika pamoja na mambo mengine ilibainisha
kwamba wizara imefanya ukaguzi katika viwanja tajwa, baada ya kupata
malalamiko juu ya uharibifu wa mazingira unaoendelea katika eneo hilo.
Na kwamba ukaguzi walioufanya umeonesha kuwa ujenzi unaofanyika
katika eneo husika hauruhusiwi na unakiuka Tangazo la Serikali (GN)
No. 76 ya mwaka 1992. Kupitia barua hiyo, wizara ilimtaka Mkurugenzi
wa Halmashauri kuchukua hatua za kubomoa/kuondoa uendelezaji batili
uliokuwa ukifanyika katika viwanja Na 2019 na 2020 Mbezi Kawe. Barua
hiyo ilisainiwa na Bwana Sadoth K. Kyaruzi, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa
Wizara.
2) Uthibitisho mwingine ni barua ya tarehe 30/9/2011 kutoka NEMC kwenda
kwa Bwana Frank Mushi. Barua husika, ilitoa maelekezo kwa Mushi kuvirudisha
katika hali yake ya kawaida, viwanja namba 2019-2020 kwa mujibu wa vifungu
55(2) (a) (e), (3) na 151 (1) ,(2) (a), (b), (3) ,(4) (b) na (f) vya Sheria ya Mazingira,
sura 191 ya mwaka 2004.
Barua husika inabainisha kwamba timu ya wataalam toka Baraza la Mazingira
(NEMC), Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi ,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam na
Manispaa ya Kinondoni ilitembelea eneo husika kufuatia malalamiko kutoka
kwa viongozi na wakazi wa Kawe Beach. Timu hiyo ilibaini kwamba eneo la Mto
Ndumbwi, pamoja na bahari lilikuwa linajazwa mawe na vifusi hali iliyosababisha
kupatikana kwa viwanja na 2019 na 2020. Ambapo ndani ya viwanja hivyo
lilikuwa linajengwa jumba kubwa kinyume kabisa na vifungu 55(2)(a) , 55(2) (b) ,
55(2)(d) na 55(2)(e) vya Sheria ya Mazingira. Ilibainika pia kuwa mikoko ilikatwa
kinyume na s.63(1) ya Sheria ya Mazingira.
Kwa mujibu wa nyaraka nilizonazo, yafuatayo yalijitokeza
i) Timu ya wataalam ilibaini kwamba, tayari Wizara ya Maliasili na Utalii ilishatoa
zuio la ujenzi katika eneo husika.
ii) Manispaa ya Kinondoni, mara kadhaa iliweka zuio la uendelezaji na kutoa amri
kwa ’mmiliki’ wa eneo husika kubomoa, lakini mmiliki huyo alipuuza amri hiyo na
kuendelea na ujenzi!
iii) Ilitolewa amri ya Mahakama, tarehe 5/4/2011 kumtaka Bwana Mushi
asiendelee na ujenzi. Amri hiyo ilipuuzwa na ujenzi ukaendelea.
Baraza la Mazingira lilimwagiza tena, Bwana Mushi:-
2) Kuvunja majengo yote yaliyoko kwenye viwanja vyenye mgogoro.
3) Ndani ya siku saba, tokea amri husika kutolewa (amri ilitolewa 30/9/2011)
awe ametoa mawe na vifusi vyote vilivyoharibu mkondo wa maji na bahari na
kuurudisha mto na bahari katika hali yake ya kawaida.
4) Ndani ya siku 30 chini ya usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii
kuhakikisha kwamba mikoko yote iliyokatwa imerudishwa katika hali iliyokuwa
awali. Kwa gharama za Bwana Mushi.
Licha ya amri zote hizo, mazuio yote hayo, matamko ya mawaziri yaliyotawaliwa
na mbwembwe nyingi, ujenzi uliendelea, nyumba imekamilika. Sasa inatumika.
Wakati kigogo huyo amehamia kwenye nyumba yake kwa matangazo na
mbwembwe, Mto Ndumbwi, bahari na mazingira kwa ujumla yameharibiwa
vibaya! Bila kusahau kuwa wananchi wengine wamebomolewa nyumba zao kwa
kutumia sheria hizo hizo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira, Sura 191 ya mwaka 2004, Fungu 57(1)
hairuhusiwi kufanya shughuli zozote za kudumu za kibinadamu ndani ya mita 60
ambazo kwa asili yake zinaweza kuhatarisha au kuathiri vibaya ulinzi na utunzaji
wa mazingira, utunzaji wa bahari, kingo za mto, bwawa au mwambao wa asili wa
ziwa.
Halikadhalika, Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 ( Sura 113) Fungu 7 (1)
(d) inabainisha kwamba eneo lolote lililo ndani ya mita 60 kutoka kingo ya mto
na bahari linatakiwa kutangazwa kama ardhi hatari au kuhifadhiwa. Na pale
inapotokea kuwa masharti ya sheria moja yanapingana na masharti ya Sheria
ya Mazingira, kuhusu mambo yanayohusu usimamizi wa mazingira, Sheria ya
Mazingira ndiyo hutumika, kwa mujibu wa Fungu 232 la sheria ya mazingira sura
Kutokana na hali hii serikali inatakiwa kujinasua katika mwendelezo wa tafsiri
wanayoipata wananchi kuwa imetekwa na kuwekwa mfukoni na watu wachache
wenye uwezo. Maana wanaona kuwa huu ni mwendelezo wa serikali kuwa
na kigugumizi pale sheria zinapovunjwa na vigogo serikalini au watu wenye
fedha wanaoshirikiana na baadhi ya viongozi wa serikali na chama tawala
kufanya ufisadi. Wameona mambo ya namna hii mara kadhaa, ikiwemo
serikali kushindwa kuwachukulia hatua waliohusika na kashfa kubwa za ufisadi
kama ’akina’ Kagoda na wenzake (EPA), Richmond na kashfa nyingine nyingi.
Kwamba sasa inazidi kuonekana dhahiri kuwa kuna watu wako juu ya sheria za
nchi, huku wanyonge wakishughulikiwa. Ni wakati mwafaka sasa kwa mawaziri
wanaohusika na masuala ya ardhi na mazingira kuwaeleza Watanzania kulikoni
wananchi wa hali ya chini kuvunjiwa nyumba zao kwa kigezo cha kuvunja
sheria wakati huo huo Mchungaji Lwakatare (kigogo) ambaye uharibifu wake
ni wa hatari kuliko hata hao waliovunjiwa akitamba mtaani kwamba yeye yuko
juu ya sheria na hakuna mamlaka yoyote yenye uwezo wa kumzuia kufanya
alichofanya!
Ni aibu kwa Taifa kuwa na viongozi wa aina hii! Viongozi ambao wako tayari
kutumia fedha, hila, mamlaka na dhamana za uongozi walizopewa, kuhalalisha
haramu, ni janga kwa mstakabali wa taifa letu!
Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Imetolewa Dar es Salaam na;
Halima Mdee (MB)
Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi
No comments:
Post a Comment