Viongozi wa Uamsho, mahakamani Zanzibar
Vurugu kisiwani Zanzibar
Viongozi
saba wa kundi la kiislamu la Uamsho leo wamefikishwa katika mahakama ya
wilaya ya Mwanakwerekwe huko kisiwani Zanzibar.
Mbele ya hakimu mkaazi wa mahakama hiyo, viongozi hao wameshtakiwa kwa kosa la kusababisha vurugu miezi miwili iliyopita.
Miongoni mwa masheikh waliopelekwa
katika mahakama ya Mwanakwerekwe iliyopo nje kidogo ya mji wa Zanzibar
ni pamoja na Sheikh Farid Hadi Suleiman, Mselem Ali Mselem, Musa juma
Issa , Suleiman Majisu pamoja na Haji Sadifa ambaye ni mkuu wa usalama
wa Uamsho.
Wakiwa kizimbani, viongozi hao wamesomewa shtaka lao la kusababisha vurugu visiwani humo tarehe 17 na 18 mwezi Agosti mwaka huu.
Mwandishi wa BBC Abubakar Famau anasema kuwa
wote kwa pamoja wamelikana shtaka hilo. Musa ali Musa ambaye ni Kamishna
polisi Zanzibar amesema viongozi hao pia wamekabiliwa na mashtaka ya
nyuma kwa sababu makosa ya jinai hayaozi.
Naye wakili wa washtakiwa hao aliiomba mahakama
iwape dhamana wateja wake kwa madai kwamba kosa linalowakabili
haliwazuii wao kupata dhamana. Wakili huyo amekwenda mbele zaidi kwa
kuomba masharti nafuu ya dhamana.
Hata hivyo, hakimu wa wilaya ameahidi kulifikiria ombi hilo kesho kutwa pindi kesi itakaposikilizwa tena.
Hatua ya kukamatwa kwa sheikh Farid na wenzake
inakuja siku kadhaa baada ya sheikh huyo kuripotiwa kuchukuliwa na watu
wasiojulikana, hali iliyozua taharuki kubwa miongoni mwa wafuasi wake
ambapo jeshi la polisi lililazimika kutumia mabomu ya machozi
kuwatawanya.
Baada ya siku tatu za kutoweka kwake, taarifa za
kuonekana kwa Sheikh Farid zilianza kuzagaa mwishoni mwa juma katika
majira ya saa nne usiku. Hali iliyosababisha kiwewe ghafla na kuuamsha
mji wa Zanzibar.
Licha ya kiongozi huo kudai kwamba alitekwa na watu wa usalama, lakini jeshi la polisi linaendelea kuikana taarifa hiyo.
Siku iliyofuatia, Sheikh alitakiwa kutoa taarifa
yeye na wenzake katika kituo cha polisi ambapo walifanyiwa mahojiano
yaliyodumu kwa zaidi ya saa tano na hatimaye kufunguliwa mashtaka.
Hivyo kufikishwa kwao mahakamani leo, wengi
wamedhani ni kwa kosa la vurugu zilizotokea wiki iliyopita, hali
iliyowaacha wengi na butwaa.
Vurugu zinazotokea mara kwa mara visiwani
Zanzibar zinaonekana kuathiri shughuli za kiuchumi ikiwemo ile ya
utalii. Kwa mujibu wa wafanyakazi wa sekta ya uchumi, tayari hali hii
imepelekea wageni wengi kusitisha safari zao kwa kuhofia usalama wao.
No comments:
Post a Comment