DRC inataka UN kuadhibu Rwanda
Sultani Makenga.
Serikali ya Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo imetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuichukulia hatua
Rwanda, kwa madai ya kusaidia waasi nchini Congo badala ya kumfuatilia
mtu mmoja kama vile kanali Sultani Makenga.
Waziri wa habari wa serikali ya Congo amesema
hayo siku moja baada ya Umoja wa Mataifa na Marekani kutangaza vikwazo
dhidi ya kiongozi wa waasi wa M23, Jenerali Makenga, vikiwemo vya
usafiri na kukamata mali yake.
Serikali
ya Marekani pia imewazua Wamarekani kujihusisha kwa namna yoyote na
Sultan Makenga, ambaye alikuwa afisa wa ngazi ya cheo cha Jenerali
katika jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Hata hivyo haijaeleweka iwapo hatua ya kukamata
mali itakuwa na athari kwani inadhaniwa kuwa Makenga huenda hana mali ya
kiasi cha kumtisha ambayo iko nchini Marekani.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa, imesema waasi
wamekuwa wakipata silaha kinyume na amri ya Umoja wa Mataifa inayozuia
biashara ya silaha kuingia nchini humo.
Taarifa hiyo pia imemtaja Jenerali Makenga
kuhusika na vitendo vya mauaji, ukataji viungo vya binadamu, ubakaji,
utekaji nyara dhidi ya raia na kuwalazimisha watu kuyakimbia makaazi
yao.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa,
Susan Rice, amesema vikwazo vipya vinaonyesha kuwa dunia haitavumilia
vitendo vya uhalifu vilivyofanyika chini ya amri ya Jenerali Makenga.
Uasi ulianza mwezi March wakati wanajeshi waasi
walipojitoa kutoka jeshi la Congo na kutwaa miji karibu na Goma, mji
mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa Congo.
Maafisa walioasi walipinga kuhamishiwa katika
maeneo mengi ya nchi wakisema wanataka kubakia katika eneo la mashariki
kwa madai ya kuwalinda wananchi wa eneo hilo.
Pia wanasema wanataka wakimbizi wanaoishi Rwanda, Uganda na Burundi, kupelekwa katika eneo hilo.
Umoja wa Mataifa umezishutumu Rwanda na Uganda kwa kuwaunga mkono waasi, shutuma ambazo nchi zote mbili zimekana kuhusika
No comments:
Post a Comment