Jeshi la Nigeria
limetuhumiwa kufanya vitendo vya kukiuka haki za bindamu katika harakati
zao dhidi ya kundi haramu la Boko Haram.
Madai haya yametolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International.
Shirika hilo limesema katika ripoti
yake kuwa ukiukwaji unaofanywa na wanajeshi ni pamoja na mauaji ya
kiholela, utekaji nyara na mateso.
Msemaji wa jeshi la Nigeria amekanusha madai hayo akisema kuwa wanajeshi hufanya kazi yao kwa kuzingatia sheria.
Harakati za kundi la Boko Haram, wanaopigania sheria za kiisilamu pia zimesababisha vifo vya mamia ya watu mwaka huu.
Wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara kaskazini mwa Nigeria na maeneo ya kati mwa Nigeria mwaka 2009.
Katika ripoti yake shirika la Amnesty limelaumu
Boko Haram kwa visa vingi vya ukiukwaji wa haki za binadamu mauaji,
kuteketeza makanisa na shule na mashambulizi yao dhidi ya waandishi wa
habari.
Lakini ilisema kuwa hatua za jeshi dhidi ya kundi hilo zimechochea hali ya vurugu kuwa mbaya zaidi.
" Hali ya mashambulizi na mashambulizi ya
kulipiza kisasi imehusisha vurugu kutoka pande zote athari zake zikiwa
mbaya zaidi dhidi ya haki za watu hususan wale walionaswa katika vita
hivi’’ alisema katibu mkuu wa shirika hilo Salil Shetty.
"Watu wanaishi kwa hofu ya mashambulizi kutoka
kwa Boko Haram na kufanyiwa vitendo vya dhulma mikononi mwa jeshi ambalo
linapaswa kuwalinda’’ aliongeza Shetty.
Kwa mujibu wa Amnesty, visa vya watu kupigwa
risasi na wanajeshi au kupigwa hadi kufa wakati wakizuiliwa ni kawaida
katika eneo la Kaskazini mashariki mwa nchi.
Amnesty linanukuu kile ilichosema ni watu
kuendelea kuishi kwa hofu ambapo hata wanaogopa kuripoti uhalifu na
waandishi nao wanapuuza kuripoti taarifa hizo.
Amnesty Inataka serikali kuelezea ukweli kuhusu
matukio ambayo yamehusisha jeshi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya
wanaofanya udhalimu huo
No comments:
Post a Comment