Mapigano mapya Congo
Mapigano mapya yamezuka
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kati ya wanajeshi
wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na waasi wa M23,na kuwalazimisha
watu kukimbia makaazi yao.
Mwandishi wa BBC katika eneo la tukio amesema
kumekuwa na mapigano makali ya silaha kaskazini mwa mji mkuu wa jimbo la
Kivu kaskazini, Goma.
Watu wapato 50,000 hawana mahali pa kuishi tangu mwezi Aprili wakati waasi walipoasi jeshi.
Umoja wa Mataifa unazishtumu Rwanda na Uganda kwa kuwaunga mkono waasi, shutuma ambazo zinapingwa na nchi zote mbili.
Mwandishi wa BBC, Gabriel Gatehouse amesema-
kuzunguka kijiji cha Kibumba kiasi cha kilomita 30 kaskazini mwa Goma
-hali imekuwa mbaya zaidi tangu mwezi Julai.
Amesema serikali imepeleka vikosi zaidi, katika
eneo hilo ikiwa ni pamoja na helikopta za kijeshi, pia askari wa kulinda
amani wa Umoja wa Mataifa wameonekana katika maeneo ya kijiji cha
Kibumba.
Msemaji wa jeshi la serikali mjini Goma, Olivier
Hamuli, amesema wapiganaji waasi 44 wameuawa na afisa mmoja wa cheo cha
juu katika jeshi la serikali pia ameuawa.
Pande zote mbili wamelaumiana kwa kuanzisha mapigano hayo yaliyoanza mapema asubuhi Alhamisi.
Mwandishi wetu amesema wakati alipokuwa katika
eneo linalodhibitiwa na waasi Jumatano, aliwaona waasi wa M23 -ambao pia
hujulikana kama Jeshi la Ukombozi la Congo wakisambaza askari wake na
kujiandaa kwa vita.
Watu wanakimbilia kuelekea kusini ambako majeshi ya serikali yanadhibiti maeneo hayo wakiwa wamebeba mizigo yao vichwani.
Baadhi yao wamekuwa wakienda katika kambi kubwa ya Kibai iliyopo katika vitongoji vya kaskazini mwa Goma.
Msema wa Umoja wa Mataifanchini Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo, Luteni Kanali Prosper Basse, amesema pia kumekuwa
na mapigano kilomita 90 kaskazini mwa Goma, huku majeshi ya serikali
yakitwaa mji wa Mabenga na kusonga mbele kuelekea mji wa Kiwanja ambao
ni mji muhimu wa waasi.
No comments:
Post a Comment