Muda wayoyoma kwa M23


Generali Sultani Makenga , kiongozi wa M23

Kiongozi wa kisiasa wa kundi la waasi la M23 yuko mjini Kampala kwa mkutano na wakuu wa majeshi kanda ya maziwa makuu.

Msemaji wa kundi hilo, aliambia BBC kuwa mkutano huo utaangazia ikiwa waasi hao wataondoka katika mji wa Goma.

Waasi wa M23 ni wanajeshi walioasi jeshi la Congo mwezi Aprili , na wanasema kuwa serikali imekataa kutimiza baadhi ya makubaliano waliyoafikia mwezi Machi mwaka 2009.

Uganda imekuwa ikipatanisha waasi hao na serikali ya DRC tangu mwezi Agosti.

Mwandishi wa BBC mjini Kampala Cathrene Byaruhanga anasema kuwa waasi hao wana hadi mwishoni mwa leo kuondoka Goma.

Hali ya usalama mjini Goma ni tete huku maelfu wakitoroka mwakao

Hii ndio amri iliyotolewa na viongozi wa kikanda siku ya Jumamosi.

Majirani wa Congo, wakiongozwa na Uganda wanajaribu kuzima uasi huo Mashariki mwa nchi. Kufuatia mkutano uliofanyika mwishoni mwa Juma, viongozi wa maziwa makuu waliwasihi waasi hao kundoka Goma kabla ya kuanza kwa mazungumzo nao.

Rais Joseph Kabila, alikutana na waasi hao pia mwishoni mwa wiki lakini akasisitiza kuwa mazungumzo hayajaanza.

Waasi wanasema wangalia wanatathmini hatua za kuchukua.

Hata hivyo jeshi la Uganda lilikataa kuthibitisha ikiwa kiongozi huyo, Brigedia Generali Sultani Makenga yuko mjini Kampala.

Baraza la usalama la umoja wa Mataifa lilimwekea vikwazo vya usafiri wiki mbili zilizopita kwa sababu ya harakati za waasi hao Mashariki mwa Congo.

No comments:

Post a Comment