*Kundi kubwa la askari lazingira mahakama
*Amri ya kumfutia dhamana yaendelea
*Amri ya kumfutia dhamana yaendelea
Sheikh Ponda Issa Ponda akifungwa pingu na askari
Magereza baada ya kesi inayomkabili na wenzake 49 kuahirishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana.
Ulinzi mkali jana
uliimarishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam
kabla ya kesi inayomkabili Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49
kutajwa.
Ponda na wenzake hao wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo kula
njama, kuingia, kujimilikisha ardhi kwa jinai, wizi wa mali ya Sh.
milioni 59.6. Sheikh huyo pia anakabiliwa na shtaka la kufanya uchochezi
wa kuhamasisha wafuasi wake kutenda makosa.
WATU WAKAGULIWA KWA MITAMBO
NIPASHE lilishuhudia watu waliokuwa wakipita kwenye lango la kuingilia
mahakamani hapo kila mmoja akifanyiwa upekuzi kwa kutumia mitambo maalum
ya CCTV.
Vile vile, lilishuhudia makachero waliovaa kiraia ambao haikujulikana
kama wanatoka kwenye majeshi ya ulinzi na usalama wa raia au la, wakiwa
wametanda katika maeneo mbalimbali ya Mahakama hiyo ili kuhakikisha
yanakuwa na amani na utulivu kabla na baada ya washtakiwa hao kufikishwa
mahakamani hapo.
Kadhalika, kulikuwa na ulinzi wa askari polisi na magereza waliovaa vifaa maalum, vikosi vya mbwa na farasi.
Ilipofika majira ya saa 2:00 asubuhi, askari ambao idadi yao
haikujulikana waliovaa sare za polisi na magereza, walisambaa katika
viunga vya mahakama hiyo.
Mitambo hiyo ikiwa imefungwa karibu na geti la kuingia mahakamani hapo,
ilitumika kuchunguza kila mtu aliyekuwa akiingia na magari.
Makachero hao walizuia watu wote waliofika eneo la lango kuu la
kuingilia mahakamani hapo na kuwaruhusu wafanyakazi wa mahakama hiyo,
watu waliokuwa na kesi na waandishi wa habari.
DHAMANA YA PONDA BADO IMEFUNGWA
Baadaye saa 2:30 asubuhi, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Victoria Nonga,
aliwasomea washtakiwa 49 masharti ya dhamana isipokuwa Sheikh Ponda
ambaye ni mshtakiwa namba moja kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini
(DPP) hajaondoa pingamizi la dhamana dhidi yake.
Washtakiwa hao walitakiwa kuwa na mdhamini mmoja kila mmoja atakayesaini hati ya dhamana ya Sh. milioni moja.
Hakimu Nongwa alisema mshtakiwa atakayetimiza masharti ataachiwa kwa dhamana.
Hadi NIPASHE linaondokana mahakamani hapo, washtakiwa hao walishindwa
kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa mahabusu hadi Novemba 15,
mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.
Kabla ya kuahirisha kesi hiyo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini
Kweka, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba
Mahakama hiyo kupanga tarehe ya kuwasomea washtakiwa hao maelezo ya
awali.
Hakimu Nongwa alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 15, mwaka huu.
Oktoba 18, mwaka huu washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa
mara ya kwanza na kusomewa mashtaka, lakini DPP, aliwasilisha hati ya
kiapo cha kupinga dhamana ya Sheikh Ponda kwa usalama wake na maslahi ya
Taifa.
Washtakiwa wengine ni Kuluthumu Mohamed, Zaldah Yusuph, Juma Mpanga,
Farida Lukoko, Adamu Makilika, Athum Salim, Seleman Wajumbe, Salum
Juma, Salum Mkwasu na Ramha Hamza.
Wengine ni Halima Abas, Maua Mdumila, Fatihiya Habibu, Hussein Ally,
Shaban Ramadhani, Hamis Mohamed, Rashid Ramadhani, Yusuph Penza, Alawi
Alawi, Ramadhani Mlali, Omary Ismaili, Salma Abduratifu, Khalidi
Abdallah, Said Rashid, Feswali Bakari, Issa Wahabu, Ally Mohamed,
Mohamed Ramadhani, Abdallah Senza, Juma Hassani na Mwanaomary Makuka.
Wengine ni Omary Bakari, Rashid Ndimbu, Hamza Ramadhani, Ayubu Juma,
Maulid Namdeka, Farahan Jamal, Smalehes Mdulidi, Jumanne Mussa, Salum
Mohamed, Hamis Halidi, Dite Bilali, Amiri Said, Juma Yassin, Athuman
Rashid, Rukia Yusuph, Abubakari Juma na Ally Salehe.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa katika shtaka la kwanza, Oktoba 12, mwaka
huu huko Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote 50 walikula njama
ya kutenda makosa.
Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza, eneo la
Chang’ombe Markas, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao
kwa jinai walivamia kwa nia ya kutaka kujimilikisha kiwanja mali ya
Agritanza Ltd.
Ilidaiwa kuwa katika shtaka la tatu kuwa, kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka
huu katika eneo la Chang’ombe Markas pasipo uhalali na hali ya uvunjifu
wa amani, washtakiwa hao walijimilikisha ardhi hiyo.
Katika shtaka la nne, ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu
karika eneo hilo, washtakiwa hao waliiba vifaa mbalimbali vya ujenzi
yakiwamo matofali 1,500, tani 36 za kokoto na nondo vyenye thamani ya
Sh. 59,650,000.
Upande wa Jamhuri ulidai katika shtaka la tano kati ya Oktoba 12 na 16,
mwaka huu huko Chang’ombe Markas, Sheikh Ponda akiwa Katibu wa Jumuiya
na Taasisi za Kiislam Tanzania, aliwashawishi wafuasi wake kutenda
makosa ya jinai. Washtakiwa hao walikana mashtaka dhidi yao.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment