Waziri Kivuli wa
Nishati na Madini, John Mnyika, amesema hatua ya kufukuzwa kazi pekee
kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William
Mhando, haitoshelezi, bali yeye na wenzake alioshirikiana nao wanapaswa
kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), alisema hayo kupitia
taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari kupitia mtandao wa
kompyuta, ikiwa ni siku moja baada ya Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco,
kutangaza kumwachisha kazi Mhando baada ya kukutwa na hatia ya
ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Mnyika alisema baada ya kufukuzwa kazi, serikali inatakiwa kurejea
katika hotuba aliyoitoa bungeni kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni ya kutaka Mhando pamoja na wenzake walioshirikiana nao katika
kashfa hiyo wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Pia aliitaka Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, kueleza hatua, ambazo
imezichukua kwa watendaji wengine wa shirika hilo, ambao walishirikiana
na Mhando.
“…Na iwapo bodi hiyo haitachukua hatua za haraka, nitaiweka hadharani
taarifa ya kamati iliyoundwa na bodi hiyo kuchambua taarifa ya Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kueleza hatua zinazopaswa
kuchukuliwa na Rais Jakaya Kikwete dhidi ya bodi yenyewe,” alisema
Mnyika.
Alitaka hatua dhidi ya Mhando na wenzake waliohusika, kutogeuzwa kuwa
kafara ya kuficha uzembe na udhaifu wa serikali kwa ujumla wake, kwani
taarifa za utendaji wa Tanesco kuhusu mpango wa dharura wa umeme pamoja
na ununuzi wa mafuta uliokuwa ukifanyika, zilikuwa zikiwasilishwa kwenye
vikao vya Wizara ya Nishati na Madini na vya Baraza la Mawaziri pia.
Alisema ili ukweli wa kina ujulikane, Kambi Rasmi ya Upinzani
imependekeza Bunge liazimie kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza
masuala yote ya ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka na
tuhuma za ufisadi katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na
ununuzi wa mafuta kwa ajili ya mitambo ya umeme.
Alitaka uchunguzi huo umshirikishe CAG katika kufanya ukaguzi wa
kiuchunguzi kwa malipo yaliyofanywa na kampuni ya BP, ambayo kwa sasa ni
Puma, Oryx na Camel Oil, ili kubaini iwapo kuna vigogo zaidi wa
serikali waliojinufaisha kwa kisingizio cha dharura ya umeme.
No comments:
Post a Comment