Yanga yaishika Simba kileleni

Mshambuliaji Didier Kavumbagu wa Yanga (kushoto), akwania mpira dhidi ya beki wa Mgambo JKT, Salum Kipanga wakati wa mechi yao ya ligi kuu ya soka Tanzania bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Yanga iliifikia Simba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kushinda 3-0 dhidi ya Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kufikisha pointi 23, sawa na 'Wekundu wa Msimbazi' walioshikiliwa katika sare ya 1-1 dhidi ya timu ya mkiani ya Polisi kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro jana. 

Hata hivyo, Simba yenye wastani wa magoli 12, inaendelea kuongoza ligi kwa wastani wa goli moja zaidi ya Yanga yenye wastani wa magoli 11. Simba imefunga magoli 20 na kufungwa 8 wakati Yanga imefunga magoli 21 na kufungwa 10.

Beki wa kati Nadir Haroub 'Cannavaro' alifunga kwa kichwa katika dakika ya pili ya mchezo na washambuliaji Didier Kavumbagu na Jerry Tegete wakaongeza mengine mawili wakati Yanga ilipopata ushindi wa saba katika mechi 11 na kuwasahaulisha mashabiki wao mwanzo mbaya wa msimu uliowafanya wamfukuze kocha Mbelgiji Tom Saintfiet aliyedumu nao kwa siku 80 tu huku akiwa ameshawapa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).

Lakini mambo hayakuwa mazuri kwa mabingwa Simba ambao walitanguliwa kwa goli la dakika ya 33 kutoka kwa Mokili Lambo, aliyekuwa ameingia uwanjani dakika 5 tu zilizopita kuchukua nafasi ya John Bosco aliyepumzishwa katika dakika ya 28.

Simba walirejea kipindi cha pili wakiwa nyuma kwa goli 1-0 kabla ya kiungo wao aliye katika kiwango cha juu tangu kuanza kwa msimu huu Amri Kiemba kuwasazishia katika dakika ya 57 akimalizia kona iliyochongwa na Emmanuel Okwi.

Ilikuwa ni sare ya 5 katika mechi 7 zilizopita za Simba baada ya kushinda zote nne za kwanza mfululizo, wakati Polisi ilipata pointi yao ya tatu kutokana na sare tatu huku ikiendelea kubaki mkiani mwa ligi ikiwa haina ushindi baada ya mechi 11. Imefungwa mechi 8.

Sare nyingine katika mechi za ugenini, ilionekana kumchanganya kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic ambaye alidai kwamba refa Jacob Ondongo kutoka Mara alichezesha vibaya na kwamba alionekana kuipendelea timu ya mwenyeji.

Kocha msaidizi wa Polisi, Ally Jangalu aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri akisema walikuwa na makosa katika upande wa ufungaji lakini wamerekebisha kiwango tangu walipocheza dhidi ya Ruvu Shootings ambapo walilala 2-1 kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.

Kwenye Uwanja wa Taifa jana, Mgambo ambao waliwashikilia Simba katika sare ya kustusha mkoani Tanga iliyochangia kiungo wa Wekundu, Haruna Moshi 'Boban' kusimamishwa, walijikuta wakimaliza wakiwa 10 uwanjani baada ya beki wao Salum Mlima kumchezea rafu beki wa Yanga, Mbuyu Twite katika dakika ya 85 na kutolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro.

Coastal Union ya Tanga iliyo katika nafasi ya tatu itajaribu kuitetea nafasi yake wakati itakapocheza ugenini dhidi ya Azam iliyo katika nafasi ya nne kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi leo.

No comments:

Post a Comment