Mwili
wa marehemu Marystella Alphonce, umezuiliwa katika hospitali ya Hindu
Mandal jijini Dar es Salaam, baada ya kugundulika alipata matibabu
yaliyogharimu Shilingi milioni 7.2 kwa kutumia kadi ya kughushi ya bima
ya afya.
Hatua hiyo ilifikiwa na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) jana na kwamba kadi
iliyotumika kwa matibabu, ilikuwa mali ya mtu aliyefahamika kwa jina la
Honoratha Mageza.
Mgonjwa huyo ambaye alilazwa Novemba 12 mwaka huu katika hospitali hiyo, alifariki juzi hospitalini hapo.
Baada ya kuandaliwa hati ya kifo, ndugu wa marehemu walitaka jina lake
kubadilishwa ndipo ilipogundulika kuna ‘mchezo mchafu’ uliofanyika
wakati wa matibabu.
Wataalamu wa bima ya afya, kanda ya Ilala waliopo hospitalini hapo,
walifuatilia kadhia hiyo kwa karibu, kujua sababu za ndugu wa marehemu
Marystella kutaka kubadilisha jina kutoka Honoratha Mageza lililotumika
wakati wa matibabu.
Baada ya uchunguzi, iligundua kuwa marehemu huyo alikuwa akitumia hilo
(Honoratha Mageza), hali ambayo ingeilazimu NHIF kulipia gharama hizo
ingawa mhusika (marehemu Marystella) hakuwa mwanachama halali.
Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa NHIF, Raphael Mwamoto, alisema
wamegundua marehemu alikuwa akipatiwa matibabu kwa njia zisizo halali
kwa kutumia kadi hiyo.
Mwamoto alisema NHIF inafanya ukaguzi wa mara kwa mara katika hospitali
ambazo wanatumia bima ya afya, kuangalia huduma zinazotolewa na
kuwabaini wanaotibiwa kinyume cha sheria.
Alisema kufutia tukio, hilo walimuita mhusika wa kadi hiyo ambapo
alifika mume wa Honoratha Mageza, ambaye ni Daktari katika halmashauri
ya wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani, Dk. Jovis Magezi.
Hata hivyo, Dk Magezi alipohojiwa na wataalamu wa bima kuhusu kadi hiyo,
alijibu aliyefariki alikuwa mkewe, ingawa ilibainika si kweli.
Mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo:
Swali: Je, una uhakika aliyefariki ndiye mhusika katika hii picha ya kitambulisho cha bima?
Dk. Magezi: Ndio
Swali: Tueleze una uhusiano gani na marehemu?
DK. Magezi: Huyu ni mke wangu.
Swali: Unajua alilazwa hospitalini hapa kwa muda gani kabla ya kifo chake?
Dk Magezi: Kama wiki mbili zilizopita
Hata hivyo, ilibainika kuwa kabla ya kifo chake, Marystellah alilazwa
hospitalini hapo kwa takribani mwezi mmoja. Kisha mahojiano yakaendelea
hivi:
Swali: Una uhakika kama aliyefariki anaitwa Honoratha
na mbona haupo katika hali ya majonzi, halafu iweje usahau tarehe ambayo
alilazwa mkeo hospitali?
Dk Magezi: Ni Kweli huyo ni mke wangu
Swali : Najua unatudanganya, tutajie namba ya simu ya huyu mkeo tujue ni sawa na ile iliyoandikwa kwenye faili?
Hapo Dk Magezi hakujibu badala yake alichukua simu yake ya kiganjani na kuanza kutafuta namba.
Swali: Hivi kweli unawezaje kuisahau namba ya mkeo?
Baada ya swali hilo, Dk. Magezi alikiri kuwa aliyefariki si mkewe na
kwamba ni mdogo wa mkewe ambaye jina lake anaitwa Marystela na kuomba
suala hilo walimalize.
Baada ya hapo Mwamoto alikwenda kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi na ndipo
askari kanzu walipokuja kumkamata ili akatoe maelezo yake kufuatia kwa
tukio hilo.
Mwamoto alisema Dk. Magezi ataendelea kushikiliwa na polisi mpaka mkewe
ambaye alihusika kutoa kadi yake kwa ajili ya marehemu kupatiwa
matibabu, atakapojitokeza.
Naye, Mwanasheria wa NHIF, Margaret Malangalila, alisema kuwa mtuhumiwa
amefanya kosa la jinai kujipatia huduma kwa njia ya udanganyifu huku
akijua hairuhusiwi kufanya hivyo.
Alisema kwa mujibu wa sheria ni kwamba NHIF haitahusika kulipa deni hilo
kutokana na mkataba walioingia na hospitali hiyo, hivyo wanaendelea
kulichunguza suala hilo kubaini na wale wengine ambao wanatumia kadi ya
bima kinyume na makubaliano.
Kwa upande wake Daktari Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Kaushik Ramaiya,
alisema kuwa kutokana na tukio ambalo limejitokeza tayari wameshachukua
hatua na kuwajulisha madakatari kuhakikisha mgonjwa atayefikishwa
hospitalini hapo ndani ya saa 24 awe amewasilisha kadi yake.
Alisema wakati mwingi mgonjwa anafikishwa akiwa katika hali ambayo sio
nzuri na ndugu zake kumfungulia faili na kujikuta akitumia jina ambalo
sio la mgonjwa, huku akiendelea kupatiwa matibabu.
"Sasa pale inapotokea mgonjwa kafariki ndio utaona ndugu wanakuja na
kuanza kutaka jina la hati ya kifo libadilishwe, tukio lililotokea
limetupa funzo hivyo madakari tayari wameshaambiwa kufuatilia kwa
umakinii," alisema
Akizungumzia juu ya deni hilo alisema familia ndio itahusika kufanya
gharama hizo na kwamba kwa sasa wanachokisubiri ni kupata maelezo ya
mhusika wa kadi ya bima iliyokuwa ikitumika.
Dk. Ramaiya alisema ataenda kuzungumza na wakubwa wake kama watauruhusu
mwili huo kuchukuliwa ama la, kwani watafuata utaratibu wa kibinadamu
juu ya suala hilo.
Hata hivyo, ndugu wa marehemu hao ambao walifika tangu majira ya asubuhi kutaka kuuchukua mwili huo ilishindikana.
NIPASHE Jumamosi ilifanikiwa kuzungumza na mmoja wa ndugu wa marehemu,
alisema walifika jana kuchukua mwili huo lakini walizuiwa kutokana na
madai ya kudaiwa gharama za matibabu.
Pia mtu mmoja ambaye alikuwa katika msiba huo alieleza kuwa gari maalamu
ya kusafirishia maiti ilifika kwa ajili ya kubebe mwili huo na
kushindikana kutokana na marehemu kuwa deni.
Wakati huo huo pia Mwamoto alisema juzi walifanikiwa kumfikisha polisi
mfanyabiashara, Endrew Mjetu, ambaye alitoa kadi yake ya bima na
kumpatia Elia Jonathani anayesumbuliwa na saratani.
Alisema mgonjwa huyo ambaye anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Ocean
Road walimuambia dawa hakuna na kumjulisha duka la kwenda kununua.
Alieleza kuwa Jonathani baada ya kwenda kwenye duka la Okinawa
alijulishwa dawa hizo ni Shilingi 800,000 aliwaambia hana uwezo
kutokana na hali aliyokuwa nayo.
Mwamoto alisema kwa mujibu wa Jonathani alidai kuwa Okinawa ilimjulisha
atafute mtu mwenye kadi ya bima ya afya ili waweze kumsaidia kumpatia
dawa hizo.
Alisema kijana huyo alifanikiwa kuipata kadi hiyo na ndipo alipofika
katika ofisi ya NHIF kutaka kupata maelekezo jinsia ya kuitumia ili
aweze kupatiwa huduma.
Hata hivyo, alisema walipogundua suala hilo walitega mitego bila mgonjwa
huyo kuelewa kinachoendelea na hatimaye kumkamata mhusika wa kadi hiyo
ambaye anashikiliwa kituo cha polisi.
Mwamoto alisema kutokana na hali ya mgonjwa ilivyo walishindwa kumshilikia na kwamba jambo walilomsaidia ni kuzipata dawa hizo.
Akizungumza na waandishi Jonathani alisema anasumbuliwa na saratani ya
haja kubwa ambapo hawezi kujisaidia na alipokwenda hospitali ya Ocean
Road walimuandikia dawa na kumtaka aende katika maduka ya dawa ya
Okinawa kwenda kuzinunua.
Jonathani alisema Mjetu sio ndugu yake kwani alimuonea huruma na
kumpatia kadi hiyo na kwamba kwa sasa kinachomuumiza ni kukamatwa huku
ndugu zake wakimlamu na kutaka akamatwe.
"Najua amenisaidia naumia alivyokamtwa kwani bila yeye nisingeweza
kuzipata hizi dawa na ndugu zake wananilamu naona ni heri nikamatwe mimi
niwekwe polisi kwani ndugu hawanielewe jamani naumia kwa mambo mengi,"
alisema hayo huku akiwa analia
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alithibitisha kutokea
kwa tukio hilo na kusema watu wawili wanashikiliwa kwa uchunguzi.
No comments:
Post a Comment