Makachero
wanaofanya upekuzi kwa watu wanaoingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, jijini Dar es Salaam wakati wa usikilizwaji wa kesi inayomkabili
Sheikh Ponda Issa Ponda, jana walimkamata mganga wa kienyeji akitaka
kuingia na matunguli katika viunga vya mahakama hiyo baada ya kumfanyia
upekuzi.
Tukio hilo lilitokea jana mahakamani hapo wakati Makachero hao wakifanya
ukaguzi kwa kuwapekua watu walioingia katika viunga vya mahakama hiyo
kwa kutumia mashine maalum.
Sheikh Ponda na wenzake 49, kesi yao ilipangwa kutajwa jana na
makachero hao kama kawaida walifanya kazi wakiwa kwenye geti kuu la
kuingilia mahakamani hapo.
Saa 2:45 asubuhi mganga huyo, Rajabu Zuberi (30), mkazi wa Kijiji cha
Kelege, Muheza mkoani Tanga akiwa na mfuko mkononi, alipita eneo hilo na
makachero hao walimzuia na kuanza kumfanyia upekuzi kama watu wengine
walivyopekuliwa.
Alipokaguliwa kwa kupitishwa mashine katika mwili wake, kengele ililia
ndipo alipotakiwa kufungua mfuko huo waone kilichopo ndani,
ulipofunguliwa ndani yake kulikuwa na matunguli na vitu mbalimbali vya
uganga wa kienyeji na alipohojiwa kulikoni akajibu mzigo huo alibebeshwa
na mama mmoja mfanyabiashara.
“Mwenye mzigo ni Senorina Urassa (35) (baada ya kuona mzigo umekamatwa
alikimbilia chooni alifuatwa na kukamatwa), alikiri kumleta mganga huyo
mahakamani ili amsaidie katika kesi ya kaka yake, lakini hakumtaja
anaitwa nani,” alisema Zuberi.
Ofisa usalama huyo, alipohojiwa na NIPASHE kama mganga huyo alikuwa
anamfuata mmoja wa washtakiwa katika kesi ya Ponda, alikana kwa kusema
kwamba baada ya mahojiano na watuhumiwa walibaini kwamba hawana uhusiano
na kesi hiyo.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, alidai mbele ya Hakimu
Mkazi Victoria Nongwa anayesikiliza kesi ya Ponda kwamba mshtakiwa huyo
ameshindwa kufikishwa mahakamani kwa sababu ni mgonjwa japo hakufafanua
anasumbuliwa na maradhi gani.
“Mheshimiwa kesi ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa, lakini hatutaweza
kuendelea kwa sababu wakili wa utetezi Juma Nassoro hayupo na tumepata
taarifa kwamba mshtakiwa wa kwanza, Sheikh Ponda Issa Ponda, kashindwa
kufika mahakamani kwa sababu ni mgonjwa...mshtakiwa Ponda amebaki
mahabusu na mshtakiwa wa 50 pia ni mgonjwa yuko nyumbani, tunaomba kesi
iahirishwe,” alidai Kweka.
Hakimu Nongwa alisema kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Desemba 31, mwaka huu.
Washitakiwa wote wako nje kwa dhamana isipokuwa Ponda na Mukadam Salehe
ambao Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) aliwasilisha hati ya kuzuia
dhamana yao kwa usalama wao na maslahi ya Taifa.
No comments:
Post a Comment