WADAU mbalimbali wamepinga ombi la Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco), kuongeza bei ya nishati hiyo kwa asilimia 155
ifikapo Januari mwakani.
Pamoja na mambo mengine, wadau hao wamesema si
wakati mwafaka sasa kwa Tanesco kupandisha bei ya umeme, kwani bado ina
fursa ya kutosha kujikwamua katika matatizo yake, ikiwamo usimamizi wa
rasilimali zake na kuboresha huduma kwa wateja.
Mambo mengine ambayo wadau hao waliyataja kuwa
ni kikwazo kwa Tanesco kupandisha bei ya umeme ni rushwa ndani ya
shirika hilo, mikataba mibovu, upotevu wa umeme kuanzia vyanzo vyake
hadi kwa mteja na ukusanyaji mbovu wa madeni.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam jana katika
mkutano wa pamoja wa kupata maoni ya wadau kuhusu nia hiyo ya Tanesco,
wadau hao walisema Tanesco haina sababu ya kupandisha bei ya umeme kwani
bado inaweza kutumia rasilimali zake kujiendesha.
Tanesco imeomba
ipandishe bei ya umeme kuanzia mwakani kutokana na sababu kadhaa ikiwamo
ongezeko la gharama za uendeshaji na kukithiri kwa madeni ya shirika
hilo la umma.
“Ongezeko la bei ya umeme ambalo linawezesha
shirika kukidhi gharama za uendeshaji bila kupata faida ni asilimia 81.7
kutoka bei iliyoko sasa,” ilisema sehemu ya taarifa ya shirika hilo
iliyowasilishwa kwenye mkutano huo na Kaimu Mkurugenzi wake Mkuu,
Felchesmi Mramba.
Mramba alisema hadi Oktoba mwaka huu, Tanesco
ilikuwa inadaiwa kiasi cha Dola za Marekani 250 milioni (Sh400 bilioni),
madeni ambayo kimsingi yanachangia kurudisha nyuma maendeleo ya
shirika. Hata hivyo, Mramba hakueleza madeni ambayo shirika hilo
linawadai wateja wake ambayo yanaelezwa kuwa ni mengi yanayoweza kufidia
kwa kiwango kikubwa pengo hilo.
Katika michango yao kwa nyakati tofauti, wadau
hao walipinga maombi hayo ya Tanesco kuongeza bei ya umeme, badala yake
wakalitaka shirika hilo kuongeza ufanisi katika utendaji wake ikiwamo
kukusanya madeni kutoka kwa wateja na kutoa huduma bora kwao.
Mwakilishi
wa Shirika la Ugavi wa Umeme Zanzibar (Zeco) Mohamed Suleiman Khatib,
alisema hawakubaliani na ombi hilo la Tanesco akisema hata bei ya
iliyopo sasa inawakandamiza wakazi na wawekezaji wa Zanzibar.
“Iwapo bei hizi zitaongezwa, basi wananchi wa
Zanzibar watakuwa na maisha magumu kutokana na gharama za maisha
kuongezeka. Pia wawekezaji watahama na kukimbilia Bara ambako kutakuwa
na bei nafuu ya umeme.”
Khatib alieleza kuwa Zeco inatumia kati ya
Mega Watti 55 hadi 60 sawa na asilimia 4 ya umeme wote nchini, lakini
ripoti ya mshauri elekezi ilishindwa kumtambua kuwa ni mtumiaji mkubwa
wa umeme, hali ambayo itaibebesha mzigo mkubwa
Makamu Mwenyekiti wa
Barazala Ushauri la Ewura, Said Mohamed alisema hawakubaliani na
kupandishwa kwa bei ya umeme kwa kiwango hicho ambacho Tanesco
imekiomba.
Alisema hiyo inatokana na mshauri elekezi
kutumia kiwango cha ongezeko la asilimia 40.29 kilichoanza mwaka huu
kama msingi wa kutafuta bei mpya kwa miaka mitatu ijayo.
Katika mchanganuo wake wa miaka mitatu,
mshauri huyo elekezi alitaka bei ya wastani ya sasa iongezeke kwa
asilimia 29.49 sawa na Sh253.76 ya bei ya sasa ya Sh195 ambayo ilipangwa
kutozwa mwaka huu na alipendekeza ongezeko la asilimia 4.69 sawa na
Sh265.65 kwa mwaka 2013; asilimia 0.9 sawa na Sh268.03 kwa mwaka 2014 na
asilimia 8.64 sawa na Sh291.19 kwa mwaka 2015.
“Inaelekea mtaalamu elekezi kutoka Hispania
(AF-Mercados), aliyepewa kazi ya kutafiti gharama za Tanesco na kupanga
bei ya umeme ana uelewa au uzoefu mdogo wa kufanya kazi za namna hiyo
kwenye nchi za dunia ya tatu kama Tanzania,” alisema Mohamed.
Aidha,
baraza hilo limepinga mfumo wa bei wa moja kwa moja uliopendekezwa na
mshauri huyo elekezi likisema kuwa unakusudia kuilinda Tanesco dhidi ya
mtumiaji ambaye ni mlalahoi kutokana na bei za umeme kupanda.“Iwapo bei ya mafuta itapanda, mfumuko wa bei utaongezeka na thamani ya shilingi itashuka,” alisema Mohamed.
Akitoa mchango wake, Flaterin Kashaga kutoka
Chuo Kikuu cha Dar es salaam, alisema haoni sababu za Tanesco na Ewura
kukaa na kupanga ongezeko la bei ya umeme kwa miaka mitatu, hasa wakati
huu ambao nchi imeanza kuwa na kiwango kikubwa cha gesi.
“Mtafiti ameshindwa kutumia mazingira ya nchi
zinazoendelea kuandaa bei hiyo ya umeme, hivyo basi bei hizo
hazitarajiwi kuwakomboa maskini wa hali ya chini ambao ni asilimia 80 ya
Watanzania waishio vijijini,” alisema Kashaga.
Mwakilishi wa Shirikisho la Wenye Viwanda
Tanzania (CTI), Hussein Katemo alisema shirikisho hilo haliridhishwi na
utendaji wa Ewura na Tanesco na akapendekeza taasisi hizo ziige mfumo wa
sekta binafsi wa utawala ambao unaondoa urasimu.
Katemo alisema Tanesco haliko makini
kufuatilia madeni yake kwa sababu kila mteja anatakiwa kutoa gharama
stahiki kutokana na anavyotumia umeme, lakini madeni hayo yanazaliwa
kutokana na Tanesco kulegalega na kushindwa kujisimamia kikamilifu.
No comments:
Post a Comment