Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi
POLISI nchini wametangaza kupokea bunduki 439 na
risasi 37 kutoka kwa watu waliozisalimisha kutokana na wito uliotolewa
na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi mwezi mmoja
uliopita kuwataka wenye silaha kinyume cha sheria wazisalimishe.
Miongoni mwa silaha zilizosalimishwa na watu
hao ni pamoja na shortgun (29), gobore (352), SMG (11), Riffle (20),
bastora (22), Airgun (1), Rocket launcher (2) na SAR (2).
Msemaji wa polisi , Advera Senso alisema
katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kwamba kupatikana kwa
silaha hizo ni ushirikiano mzuri kati ya polisi na wananchi.
Senso
alisema polisi wamejipanga kwa kufanya operesheni maalumu
itakayoendeshwa nchi nzima kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola
pamoja na raia wema ili kuwabaini na kuwakamata wale wote wanaomiliki
silaha kinyume cha sheria.
Alisema operesheni hiyo itafanyika kutokana na
kumalizika kwa muda maalumu alioutoa Waziri Nchimbi kwa watu wenye
silaha kuzisalimisha bila masharti yoyote.
Hata hivyo taarifa ya Senso haikutaja ni lini operesheni ya kusaka bunduki itaanza nchini.
Alitoa
wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za mtu
ama kikundi cha watu wanaosadikiwa kujihusisha na umiliki wa silaha
isivyo halali au matukio ya uhalifu wa aina yoyote ile ili kuhakikisha
uhalifu wa kutumia silaha unapungua.”
Senso alibainisha kwamba mtu yeyote atakayetoa
taarifa za mafanikio zitakazowezesha kukamatwa kwa watu wanaomiliki
silaha kinyume cha sheria watazawadiwa Sh100,000 kulingana na mafanikio
ya taarifa aliyoitoa.
No comments:
Post a Comment