Kampuni ya Tigo yagoma kupunguza gharama za simu
logo tigo
WAKATI Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
ikiwasilisha rai ya kupunguza gharama za mwingiliano wa simu , Kampuni
ya Tigo imekataa kufanya hivyo kwa madai kuwa itahatarisha uwekezaji
wake kwa punguzo la asilimia 69.
Msimamo huo wa Tigo, umekuja baada ya TCRA
kukutana na wadau wa mawasiliano jana jijini Dar es salaam, ili
kukusanya maoni kuhusu mapendekezo ya kupunguza gharama ya mtandao mmoja
kwenda mwingine. Hatua hiyo inalenga katika kuwasaidia wananchi kumudu
gharama za mawasiliano ya simu.
Naibu Mkurugenzi wa Utekelezaji wa Kanda wa
TCRA, Victor Nkya, alisema punguzo hilo ni la kutoka asilimia 35 hadi
asilimia 69 na kwamba litaanza kutumika Machi mosi mwaka huu na kukoma
Desemba 31 mwaka 2017 .
Nkya alisema punguzo la gharama ya kupiga
mtandao mmoja kwenda mwingine kwa mwaka 2013 litakuwa asilimia 34.92,
mwaka 2014 asilimia 32.40, mwaka 2015 asilimia 30.18, mwaka 2016
asilimia 28.57 na mwaka 2017 ni asilimia 26.96.
“Lengo letu ni kupunguza gharama za
mwingiliano wa simu, mfano mwananchi ambaye yupo Tigo anapiga kwenye
mtandao wa Vodacom hizi gharama atazilipa mwenye kampuni ya Vodacom
kuilipa kampuni ya Tigo badala ya kulipa mwananchi kama ilivyo sasa,”
alisema.
Alisema maoni yanayotolewa na wadau yatachukuliwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mawasiliano na kuyafanyia kazi.
Ofisa Mdhibiti wa Kampuni ya Tigo, Levocatus
Nkata, alisema punguzo hilo ni kubwa hivyo wawekezaji watashindwa
kuendesha kampuni zao.
Alisema Kampuni ya Tigo inatoa huduma zake
hadi vijijini na kwamba hatua hiyo itaifanya ishindwe kupeleka na kutoa
huduma kwenye maeneo hayo.
Nkata alisema itachukua muda mrefu kurudisha gharama walizotumia kuendeshea kampuni yao kutokana bei ya kuendesha mitambo.
“Sisi hatukubaliani na hayo mapendekezo
yaliyoletwa na TCRA, punguzo hilo kwa sisi wawekezaji ni kubwa sana,
tunachoomba wasipunguze ibaki kama ilivyo na kwa mwaka 2017 tunaomba
ipunguze kufikia asilimia 45 tu, “alisema Nkata.
Kampuni za Airtel, Vodacom , Benson na Dovetel zimekubali punguzo hilo lakini zimeiomba TCRA ipunguze asilimia chache.
No comments:
Post a Comment