Mchina akamatwa na Takukuru akitoa rushwa kwa DC Bunda
mkuu wa wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania
(Takukuru) Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, imemkamata raia wa China, kwa
tuhuma za kutoa rushwa ya Sh. 500,000 kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, ili
kampuni yake iruhusiwe kusambaza pembejeo kwa wakulima wilayani humo.
Raia huyo wa China, Mark Wang Wei, ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Panda
International Co. Limited ya mkoani Shinyanga, ambaye alikamatwa jana
mchana katika ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo, Joshua Mirumbe, baada ya
kumuwekea mtego huo wa Takukuru.
Mirumbe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya
Wilaya hiyo, alisema Mchina huyo kupitia kampuni yake, ambayo ni ya
usambazaji wa pembejeo, juzi alimwandikia ujumbe wa simu ya mkononi
(sms) akimshukuru sana, huku akiahidi kumuona jana ofisini kwake ili
ampe zawadi.
Alisema baada ya kuahidiwa na Mchina huyo, hali hiyo ilimtia shaka kwani hakuwa na ahadi yoyote kutoka kwake.
Kutokana na hilo, alisema aliamua kuwaarifu Takukuru, ambao waliweka mtego ofisini kwa mkuu huyo wa wilaya.
“Baada ya kuahidiwa na Mchina huyo kwa kweli hali hiyo ilinistua sana na
kunitia shaka, maana mimi binafsi sikuwa na ahadi yoyote na Mchina
huyo. Sasa nilichokifanya nilimtaarifu Kamanda wa PCCB (Takukuru) na
ndipo tukaweka mtego uliofanikiwa kumtia mbaroni,” alisema.
Alisema Mchina huyo alifika jana mchana na kuingia ofisini kwake na
kumpa barua kutoka Idara ya Uhamiaji ikimtambulisha kuwa ana kibali cha
kuishi hapa nchini hadi Machi, mwaka huu.
Mirumbe alisema Mchina huyo pia alitoa Sh. 500,000 na kumpa, huku
akisema kuwa hiyo ni zawadi yake, ili airuhusu kampuni yake iweze
kusambaza pembejeo kwa wakulima wilayani hapa.
Alisema suala la usambazaji wa pembejeo linatakiwa kusimamiwa na mtu
makini, kwani msimu uliopita mawakala waliopewa jukumu hilo
walichakachua pembejeo hizo na kusababisha wakulima kutozipata kwa muda
muafaka na wengine kuzikosa kabisa.
Mirumbe alisema kufuatia hali hiyo, baadhi ya watendaji wa hamashauri
hiyo walioshirikiana na mawakala hao wamesimamishwa kazi na wengine
wameshitakiwa mahakamani, huku baadhi yao wakitorokea kusikojulikana.
Alisema hali hiyo ndiyo iliyowasukuma kuwa makini katika suala la
kupitisha mawakala wa kusambaza pembejeo wilayani hapa na kubaini kuwa
Mchina huyo alikuwa na kibali cha kumruhusu kukaa hapa nchini, ambacho
muda wake ulikuwa umebakia wa siku 10 tu.
Mirumbe alisema walichukua hatua ya kumtaka Mchina huyo, kupeleka
vitambulisho vyake kutoka Uhamiaji na sehemu zote zinazohusika.
Ilielezwa kuwa baada ya kutoa fedha hizo Takukuru walimkamata na fedha hizo kuhesabiwa mbele ya mashahidi ofisini humo.
Hadi jana jioni alikuwa akiendelea kuhojiwa na Takukuru, ambao walisema kuwa baada ya maelezo yake watamfikisha mahakamani.
Akihojiwa na waandishi wa habari, Mchina huyo alikiri kutoa fedha hizo,
huku akisema alimpa mkuu huyo wa wilaya kama zawadi yake na kwamba,
hakukusudia kutoa rushwa.
No comments:
Post a Comment