Deni la serikali linatisha

  Lafikia Sh. trilioni 22
  Naibu Waziri: Bado tunakopesheka

Mwakagenda alisema deni la taifa limeongezeka kwa dola 456.1 za Marekani,  sawa na asilimia 4.5 kwa kipindi cha  mwaka mmoja tangu 2011 na hatari ya kukua kwa deni ni nchi kutoaminika na hivyo kushindwa kukopesheka kimataifa.

Madhara mengine ambayo asasi hiyo inasema yanayotokana na deni kubwa kwa nchi, ni uwezekano wa wawekezaji kupunguza imani na mazingira ya kiuchumi na hivyo kukataa kuja nchini kuwekeza.


Mwakagenda alitaja madhara mengine yanayoweza kutokana na kukua kwa deni la taifa kuwa ni uwezekano wa kuvuruga uimara wa Shilingi ya Tanzania pamoja na baadhi ya maofisa wa serikali na watendaji kutumia mwanya wa kukopa kufanya ufisadi na kujilimbikizia mali.


Alisema takwimu za Benki Kuu ya Tanzaia (BoT) zinaonyesha kuwa deni la taifa lilipanda kutoka dola bilioni 1.83 za Marekani mwaka 2010 hadi kufikia dola bilioni 2.3 mwaka 2011 na uwiano wa pato la taifa (GDP) ulikuwa asilimia 44.4.


Mkurugenzi huyo aliishauri Tanzania kujifunza kutoka kwa baadhi ya nchi za Ulaya ambazo alisema madeni yao yamekuwa siyo endelevu.


Aliongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania ilisamehewa madeni yake yote, lakini inashangaza kuona imekopa tena kiasi kikubwa kama hicho, hali ambayo kwa sasa kinatishia kuvuruga uchumi.


“Siyo kila serikali inapokuwa na shida, cha kwanza kufikiria ni kwenda kukopa, lazima ibadilike na kuanza kufikiria namna nyingine ya kupata fedha za kufanyia maendeleo na shughuli zake nyingine," alisema Mwakagenda.  


MAJIBU YA MBENE

Wakati asasi hiyo ikitoa kauli za kuikosoa serikali kwa matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi, Naibu wa Fedha, Janet Mbene, jana alijibu hoja hizo akisema kuwa bado Tanzania inakopesheka na taasisi za kimataifa zikiwamo Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Akizungumza na NIPASHE, Mbene alisema kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo inaweza kuzitumia kuweka rehani ili ipate mikopo na haijafikia hatua ya serikali ishindwe kukopesheka na kupinga madai yaliyotolewa na Mwakagenda.


Naibu Waziri huyo alisema kuwa fedha zote zilizokopwa na serikali zilitumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli, kuwekeza katika sekta za elimu, afya na kukuza uchumi.


Alifafanua kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa haraka na IMF na WB wametoa ripoti inayosifia juhudi za serikali katika kukuza uchumi wake.

Kuhusu serikali kukopa fedha kutoka katika benki za ndani, Mbene alikiri kuwapo utaratibu huo, lakini alisema suala la kukopa siyo kosa kama mkopaji analipa  deni analokopa.

“Ni kweli tunachukua fedha, lakini tunafanya hivyo tukiwa tunaendelea kukusanya mapato yetu na tunapopata tunaenda kulipa deni na serikali haiwezi kuwa na fedha muda wote,” alisema Mbene.


Hata hivyo, Mbene alisema serikali ina akiba ya fedha zinazofikia Shilingi trilioni nne na kwamba kiasi hicho kinatosha kuendesha nchi na kutekeleza shughuli mbalimbali.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment