Radi yaua Mzungu akipanda Kilimanjaro

Mtalii raia wa Ireland, Ian Mc Keever (42), amefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa baadhi yao vibaya baada ya kupigwa na radi wakati wakipanda Mlima Kilimanjaro.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Pascal Shelutete, mtalii huyo alifariki dunia juzi, akiwa na wenzake 21 wakati wakipanda mlima huo kupitia njia ya Londorosi wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro.


Alisema mtalii huyo mwanaume, alikutwa na umauti hayo wakati akiwa njiani kuelekea kituo cha Kibo Moir na alifika nchini kwa shughuli za utalii wa kupanda mlima huo mrefu kuliko yote Afrika mwishoni mwa Desemba, mwaka jana.


“Walianza safari ya kupanda mlima Desemba 30, mwaka jana, kwa kampuni ya utalii ya mkoani Arusha kutokana na ajali hii wageni wengine 21 wamesitisha safari ya kupanda mlima huo,” alisema.


Shelutete aliongeza kuwa Tanapa kwa kushirikiana na kampuni ya utalii aliyotumia mzungu huyo, wanaendelea na taratibu mbalimbali za kushughulikia ajali hiyo pamoja na matibabu kwa waliojeruhiwa.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alipoulizwa juu ya tukio hilo, alisema hana taarifa na kuomba apewe muda zaidi wa kufuatilia.


Katika hatua nyingine, mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Nyabichenguche Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Nyarero Marwa (20), amekufa papo hapo baada ya kupigwa na radi akiwa amejikinga na mvua katika kijiji cha Rebu.


Ndugu yake, James Omahe, alijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime.


Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Tarime/ Rorya, Justus Kamugisha, alisema kuwa mwanafunzi huyo alipigwa na radi jioni akiwa amejikinga mvua na wenzake akiwamo ndugu yake, James Omahe kijijini hapo.


Alisema mwanafunzi huyo alikufa wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime.

No comments:

Post a Comment