Mwanafunzi auawa kwa kisu Mkuranga
MWANAFUNZI wa kidato cha pili katika shule ya Sekondari
ya Kiparang’anda wilayani Mkuranga mkoani Pwani, Ismail Mohamed (15),
amefariki baada ya kuchomwa kisu na kijana mwenzake, Ramadhani Mkamba
(19), wakati wa mkesha wa Mwaka Mpya.
Tukio hilo lilitokea saa 5:20, usiku wa mkesha wa
mwaka katika eneo la CCM II Mbagala Kiburugwa, maarufu kama Magenge 20,
tukio ambalo chanzo chake ni Sh200.
Akisimulia tukio hilo, katika Kituo cha Polisi
Mbagala Kizuiani (Maturubai), Mjomba wa Marehemu, Nurdin Mohamed
aliliambia Mwananchi, lililoambatana na kikosi cha doria cha Polisi
Temeke kuwa mtuhumiwa alimchoma kisu Mohamed kifuani, baada ya kumnyima
Sh200.
Alisema Mohamed ambaye alikuwa amefika nyumbani
kwake hapo kwa ajili ya likizo, alikutana na mtuhumiwa huyo wakati
akitoka magengeni ambapo walikuwa wakifanya biashara ya kuuza samaki.
Alisema mtuhumiwa alimwomba Mohamed Sh200 lakini
alisema hana, mtuhumiwa alimpora simu yenye thamani ya Sh20,000, halafu
akamchoma kisu kifuani kisha akakimbia.
Alisema baada ya mtuhumiwa kumchoma kisu Mohamed
na kukimbia, yeye alimchukua majeruhi na kumpeleka katika Kituo cha
Polisi Mbagala Kizuiani, ili aweze kupata fomu namba 3 ya Polisi kwa
ajili ya matibabu, lakini wakati taratibu za kupata fomu hiyo
zikiendelea, majeruhi alifariki.
Mtuhumiwa alifuatiliwa na kikosi cha doria ambacho kilifanikiwa kumtia mbaroni na kumfikisha kituoni hapo.
Katika tukio lingine, dereva teksi mmoja
aliyefahamika kwa jina la Daniel Magori anayekadiriwa kuwa na umri wa
miaka 35 na 40, amenusurika kifo baada ya kuchomwa kisu tumboni na
majambazi na kisha kumpora gari.
Tukio hilo lilitokea kati ya saa 6:15 na saa 6:30, usiku wa kuamkia Mwaka Mpya , katika eneo la Imasko wilayani Temeke.
Baadhi ya wananchi walishauri Watanzania kuwa makini hasa katika nyakati za sikukuu ili kuepuka hali kama hizo.
No comments:
Post a Comment