Mahakamani kwa kubaka mwanafunzi
Mahakama
KADA maarufu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Shafii Yatera (40), ameuanza vibaya mwaka 2013
baada ya kusherehekea Mwaka Mpya akiwa Gereza Kuu la Karanga mjini
Moshi.
Yatera alipandishwa kizimbani juzi mbele ya Hakimu mkazi, Sophia Masati
akikabiliwa na tuhuma za kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 17 ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Msasani.
Kada huyo ndiye ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa
2010 alichuana na Mbunge wa sasa wa Jimbo la Mwanga ambaye pia ni Waziri
wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na kushika nafasi ya pili.
Akimsomea mashtaka yake, Wakili wa Serikali Kanda
ya Moshi, Oscar Ngole alidai kuwa Novemba 1,2012, mshtakiwa alimwingilia
kimwili mwanafunzi huyo wa Kidato cha Nne kinyume cha sheria.
Wakili huyo alidai kuwa kitendo alichokifanya
mtuhumiwa huyo ni kinyume cha kifungu 130 (2) (e) na 131 cha kanuni ya
adhabu sura ya 16, adhabu ya kosa hilo ni kifungo cha miaka 30 jela.
Hata hivyo kada huyo wa Chadema ambaye ni mkazi wa Pasua mjini Moshi
alikanusha mashtaka hayo lakini upande wa mashtaka ukaiomba mahakama
kuzuia dhamana kwa sababu za kiupelelezi.
Wakili Ngole, alidai kuwa endapo mshtakiwa atakuwa
nje kwa dhamana ataathiri uchunguzi wa kesi hiyo kwa kile kinachodaiwa
amekuwa akimshawishi mwanafunzi huyo kutokutoa ushirikiano kwa polisi.
Hakimu Masati anayeisikiliza kesi hiyo alilikubali
ombi hilo la upande wa mashtaka na kuamuru mshtakiwa apelekwe rumande
katika Gereza Kuu la Karanga hadi Januari 14, 2013 kesi hiyo
itakapotajwa tena.
No comments:
Post a Comment