Polisi waliokwapua 150 M/- wako kazini

  Wana vyeo vya Sajini Taji na Koplo
  Kamanda Kova akwepa kueleza waliko
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova

Askari watano wanaotuhumiwa kuhusika na upotevu wa Sh. milioni 150 zilizoporwa katika tukio la ujambazi eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam wanaendelea na kazi kama kawaida huku Jeshi la Polisi likipata kigugumizi kwa kushindwa kuweka wazi majina yao.

Taarifa ambazo NIPASHE imezipata kutoka kituo cha polisi Kati (Central) jijini hapa, zimeeleza kuwa siku mbili baada ya siri kuvuja kwamba askari waligawana fedha hizo zilizodondoshwa na majambazi waliitwa na kuhojiwa kituoni hapo.


Taarifa zinaeleza kuwa baada ya kuhojiwa baadhi ya askari hao walikutwa na kiasi fulani cha fedha ambazo inasadikiwa kuwa ni sehemu ya Sh. milioni 150 zilizopotea katika mazingira ya kutatanisha wakati wa tukio la ujambazi.


Hata hivyo, tangu askari hao waitwe na kuhojiwa, inaeleza kuwa kila siku wamekuwa wakienda Kituo Kikuu cha Polisi na kusaini kitabu cha mahudhurio kwamba wapo kazini.


Hali hiyo imewashangaza askari wengine ambao wamekuwa wakihoji inakuwaje wenzao waliotuhumiwa kuiba fedha hizo wanaendelea na kazi wakati wengine wakifanya makosa kama hayo husimamishwa kazi.


Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipoulizwa na NIPASHE jana kuhusu kinachoendelea kuhusu askari hao na kwanini majina yao hayawekwi wazi kama ilivyo kwa watuhumiwa wengine.


Kamanda Kova alisema suala la askari hao hapendi kuliongelea kupitia simu na kuahidi kuwa atalitolea maelezo kwa kuitisha mkutano na waandishi, hata hivyo hakueleza lini atafanya mkutano huo.


“Suala la askari hao nitaitisha ‘press conference’, siku hizi sipendi kuliongelea jambo lolote kwa simu nimegundua kuna baadhi ya waandishi wanapenda kunilisha maneno ambayo sikuyasema,” alisema Kamanda Kova.


Hata hivyo, wakati Kamanda Kova akikwepa kuweka wazi majina ya askari hao, NIPASHE imefanikiwa kuyapata. Ingawa kwa sasa bado tunasitiri majina yao kwa kuwa hatujafakiniwa kuwapata ili wazungumzie tuhuma zinazowahusu, vyeo vyao ni kama ifuatavyo; Sajini Taji (SSGT) mmoja na wanne wana vyeo vya Koplo.


Kamanda Kova alipoitisha mkutano wa waandishi wa habari Januari 11 mwaka huu, hakutaja majina ya askari aliodai wametiwa mbaroni badala yake alitaja tu majina ya watuhumiwa wengine wawili raia wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo la ujambazi.


Watu hao aliowataja alidai ni Deogratias Kimaro (30), mkazi wa Karakata na Kulwa Mwakabala (30) mkazi wa Kijiwesamli Ilala.


Hata hivyo, alidai askari hao watano wanashikiliwa kutokana na uchunguzi wa kina uliofanywa na jopo la upelelezi likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Kanda hiyo, Ahmed Msangi.


Alisema baada ya tukio hilo zilipatikana taarifa kwamba fedha hizo zilipotea baada ya mtuhumiwa Augustino Kayula au Frank Mwangiba, kukamatwa akiwa na bastola aina ya Browning bila fedha zilizoporwa wakati inasemekana ndiye aliyepora fedha hizo akiwa na wenzake.


“Askari hawa tunawashikilia na tayari mashitaka ya kijeshi yameanza huku uchunguzi ukiendelea na utakapokamilika, tutapeleka jalada kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua za kisheria ili kuleta uwazi na uwajibikaji ndani ya jamii yetu,” alidai Kova wiki iliyopita.


Alisema baada ya tukio hilo kulikuwa na taarifa zenye kutuhumu askari hao juu ya upotevu wa fedha hizo na ndipo uchunguzi ulipoendelea ili kubaini ukweli.


Kamanda Kova aliunda jopo la wapelelezi watano lililoongozwa na Msangi kuchunguza tuhuma zinazowahusu askari hao kugawana Sh. milioni 150 za tukio la ujambazi uliotokea Kariakoo.


Alisema endapo itabainika kwamba tuhuma hizo ni za kweli wale wote waliohusika ikiwa ni pamoja na askari watachukuliwa hatua kali za kisheria.


Wakati wa tukio hilo, mbali na kuporwa kiasi hicho cha fedha pia watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi na kuwajeruhi wengine watatu.


Baada ya kutokea kwa tukio hilo, kulizuka tetesi kuwa askari waliokuwapo katika tukio hilo walichukua fedha hizo zilizodondoshwa na majambazi na kugawana katika moja ya nyumba iliyopo eneo la Jangwani.

 

No comments:

Post a Comment