Sumu’ ya DK Slaa yaitesa CCM Moshi
Dk Slaa
SASA ni dhahiri sumu aliyoimwaga Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa na makada wengine wa chama hicho mjini Moshi
wiki iliyopita, imeanza kukitafuna Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Jimbo la Moshi Mjini, limekuwa likishikiliwa na
kambi ya upinzani tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995,
huku Chadema kikiigaragaza CCM katika kiti cha ubunge mara tatu
mfululizo.
Makada wa CCM wamejitokeza na kuhoji ukimya huo wa
CCM wakati sumu hiyo imeanza kusambaa kwa kasi miongoni mwa wananchi na
kukiweka chama hicho njiapanda uchaguzi mkuu 2015.
Kada wa CCM, Ramadhan Mwindad ‘Gadaffi’ jana
alizua kizaazaa katika ofisi za CCM Moshi Mjini, alipoamua kujitoa
mhanga na kwenda kuwahoji viongozi sababu za kutojibu mapigo. Tukio hilo
lililovuta hisia za watu wengi, lilisababisha kada huyo na kiongozi
mmoja wa CCM ngazi ya wilaya kushindwa kujibu hoja na kudai kada huyo
ametumwa na Chadema.
Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lilitokea
mbele ya Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Paul
Matemu na Katibu Mwenezi wa Mkoa huo ambaye pia ni Diwani, Michael
Mwita.
“Mimi ni kada wa CCM nimekwenda pale saa 8:00
mchana huu (jana) na kuwauliza kwa nini kila siku mnafanya vikao vya
ndani vya kikatiba, lakini hamwendi kwa wananchi kujibu mapigo?”alisema.
Badala yake, kada huyo alisema kiongozi huyo ngazi
ya wilaya alimjia juu na kumtuhumu kuwa ametumwa na Chadema kuhoji
mambo hayo na kukwepa kabisa kujibu hoja ya msingi.
“Viongozi wa kitaifa wametukanwa na kudhalilishwa
sana.Mkuu wetu wa mkoa mpaka imefikia mahali ameitwa ki model
(mwanamitindo) bado viongozi wetu wamekaa kimya,”alisema.
Kauli hiyo iliungwa mkono na kada mwingine wa CCM
Kata ya Longuo, ambaye alisema baadhi ya viongozi walijinadi kwa
mbwembwe katika uchaguzi uliopita lakini sasa wanachama hawaoni makeke
yao.
“Kuna viongozi walijinadi kwa wapiga kura kuwa
oooh hili ni jembe mchagueni, mbona kimya? Hata kujibu tu matusi na
kejeli za mkutano ule wa Chadema wameshindwa”alisema kada huyo.
Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini, Elizabeth Minde alipoulizwa jana kuhusu
madai ya wanachama wake alisema yuko kwenye kikao na pindi atakapomaliza
tu angelipigia gazeti hili kutoa ufafanuzi.
Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Mwita
alipoulizwa kuhusu tafrani hiyo alisema hakuona kama kulikuwa na
mabishano katika ofisi hizo za CCM kwa kuwa alikuwa mbali kidogo na eneo
la tukio.
“Nilimwona Gadaffi na (jina la kiongozi wa wilaya)
wakizungumza ila sikujua wanazungumzia nini, lakini nataka ifahamike
CCM ina utaratibu wake wa kuitisha mikutano na hatujibu matusi,”
alisema.
Mwita alisisitiza kuwa kamwe CCM haiwezi kujibu hoja kwa
kusukumwa na mikutano ya Chadema bali watafanya hivyo kunapokuwa na hoja
na CCM iko katika mchakato wa kujibu mapigo.
Katika mkutano huo, Dk Slaa, Mbunge wa Arumeru
Mashariki, Joshua Nassari na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema
(Bavicha), John Heche walimwaga sumu inayokifanya CCM kuweweseka.
Katika mkutano huo viongozi hao pamoja na Mbunge
wa Arusha mjini, Godbless Lema wanadaiwa kutumia maneno makali
kumshambulia Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama.
Viongozi hao wa Chadema waliwachongea Gama,
Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Bernadette Kinabo na Mkuu wa Wilaya ya
Moshi, Ibrahim Msengi kuwa wanaingilia utendaji wa Halmashauri.
Kauli za viongozi hao zilitokana na hotuba ya Meya
wa Manispaa ya Moshi kuwashtaki viongozi hao wa serikali ya CCM kuwa
wanazuia utekelezaji wa maamuzi ya baraza kwa masilahi ya kisiasa.
Meya huyo alisema viongozi hao wamekuwa wakitumia
vibaya vikao vya ushauri mkoa (RCC) na vile vya wilaya(DCC) kuingilia
uamuzi halali wa Manispaa ya Moshi inayoongozwa na Chadema.
Alitoa mfano wa viongozi hao kumwagiza Mkurugenzi
wa Manispaa hiyo, Bernadette Kinabo kuendesha operesheni dhidi ya
wafanyabiashara wadogo ili kuichonganisha Chadema na wananchi.
Kwa mujibu wa Meya huyo, Baraza la Madiwani la
Halmashauri hiyo limekuwa katika wakati mgumu kutokana na Kinabo kukataa
kutekeleza maazimio ya vikao halali ili tu kuinufaisha CCM kisiasa.
Mathalan alisema, sera ya Chadema Moshi Mjini ni
kuwalipia ada wanafunzi wote wa sekondari ambao wazazi wao hawana uwezo,
lakini mkurugenzi huyo amekataa kuidhinisha fedha hizo.
Meya huyo alisema mwaka 2011/2012, Halmashauri
hiyo inayoongozwa na Chadema ilitenga Sh196 milioni kulipa ada hizo na
mwaka 2012/2013 imetenga Sh216 milioni ambazo zote hazijaidhinishwa.
“Ukimuuliza anasema sera ya elimu bure siyo sera
ya Serikali.Tunaomba hoja hiyo uipeleke bungeni tujue ni wakati gani
vyama vinaweza kutekeleza sera zake kwa halmashauri
inazoziongoza,”alisema.
Meya huyo alisema vitendo vinavyofanywa na
viongozi hao wawili ni dhahiri vina lengo la kuidhoofisha Chadema
kisiasa katika Jimbo la Moshi na pia kuwagombanisha na wananchi.
No comments:
Post a Comment