Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi
SAKATA la dawa bandia za kupunguza makali ya
Ukimwi (ARV) lililosababisha Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) na
wenzake wawili kusimamishwa kazi, liko kwa Mkurugenzi wa Mashitaka
Nchini (DPP).
Hayo yalielezwa mwishoni mwa juma kwenye Kamati ya
Bunge ya Kudumu ya Huduma za Jamii na Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii, Dk Hussein Mwinyi.
Dk Mwinyi alisema baada ya uchunguzi wa kina, suala hilo sasa limefikishwa kwa DPP kwa hatua zaidi.
“Tunasubiri uamuzi wa DPP baada ya wizara yangu
kuchukua hatua za awali za kumsimamisha Mkurugenzi Joseph Mgaya, baada
ya kubainika kuwapo na kusambaa ARV bandia,” alisema Dk Mwinyi.
Dk Mwingi alisema mbali na mkurugenzi huyo pia
wizara yake iliwasimamisha kazi Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora, Daud
Maselo na Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora wa Dawa, Sadick Materu.
Pamoja na kuchukua hatua ya kusitisha Kiwanda cha TPI kuzalisha dawa
hizo.
“Wizara iliwasimamisha kazi viongozi hao ili
kupisha uchunguzi kufuatia kuruhusu kusambazwa kwa dawa bandia za
kupunguza makali ya Ukimwi aina ya TT –VIR 30 katika vituo mbalimbali
vya kutolea huduma za afya nchini. Sasa suala lao limeshafikishwa kwa
DPP kwa hatua zaidi za kisheria, tunasubiri uamuzi wake,” alisema Dk
Mwinyi.
Alisema pia wamepiga marufuku usambazaji na
matumizi ya dawa aina ya TT –VIR 30 toleo namba 0C .01.85
inayotengenezwa na TPI, kutokana na dawa hiyo kutengenezwa chini ya
kiwango na kutofaa kwa matumizi ya binadamu.
Alisema hatua hiyo ya wizara ilichukuliwa baada ya
kubaini kuwepo kwa dawa hizo katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime,
kufuatia ukaguzi uliofanywa na Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Chakula
na Dawa Nchini (TFDA).
“Mheshimiwa mwenyekiti kufuatia ukaguzi na
ufuatiliaji uliofanywa, pamoja na uchunguzi wa kimaabara ulibaini mengi
ikiwa ni pamoja na nyaraka zilizokutwa MSD zinaonesha kuwa TPI kuiuzia
MSD dawa hiyo bandia,” alisema.
Dk Mwinyi alisema Serikali inahakikisha kuwa dawa
zenye ubora unaotakiwa za kupunguza makali ya Ukimwi zinaendelea
kupatikana katika vituo vya kutolea huduma hiyo.
No comments:
Post a Comment