Lowassa anusurika kifo ajali ya gari

Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa. 


WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amenusurika kifo baada ya gari lake alilokuwa akisafiria kutoka jijini Dar es Salaam kwenda mkoani Morogoro, kupata ajali.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa Lowassa alipata ajali hiyo jana saa 2:00 asubuhi baada ya gari lake hilo kugongwa na basi la Moro Best eneo la Bwawani mkoani humo.

Kwa mujibu wa habari hizo ajali hiyo ilitokea baada ya basi la Moro Best lililokuwa likitokea Morogoro kuelekea Dar es Salaam, kujaribu kuyapita mabasi kadhaa na kukutana na gari la Lowassa kisha kuligonga ubavuni.

Hata hivyo, katika ajali hiyo hakuna aliyejeruhiwa na Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli, aliendelea na msafara yake.

Lowassa alikuwa anaelekea Morogoro ambako pamoja na mambo mengine, alishiriki harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Kilakala.

Akizungumzia ajali hiyo kabla ya kufanyika harambee hiyo, Lowassa  aliwaeleza waumini kuwa kunusurika kwake katika ajali hiyo ni kwa neema za Mungu tu.

“Mkono wa Mungu ni mkubwa, bila ya hivyo  simulizi zingekuwa nyingine juu yangu. Wakati nilipoliona basi likiwa linakuja upande wetu kutugonga, ulinijia wimbo mmoja unaosema ‘’Hivi haya yote ya nini, ni huruma tu,’’ alisema Lowassa.

Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa Usalama Barabarani (RTO), Mkoa wa Morogoro, Leonard Gindo alisema taarifa za tukio hilo walizisikia na kuamua kufika eneo la ajali na kukuta vioo vilivyopasuka bila magari kuwepo.

“Hakuna taarifa iliyoripotiwa, lakini tukio hilo lilitokea na kwamba tulifika eneo la tukio na kukuta vioo tu. Inaelezwa kilichotokea ni basi la Moro Best kujaribu kulipita basi lingine na ghafla gari la Lowassa nalo lilikuwa linakuja kwa mbele,” alisema Gindo.

Alisema kuwa taarifa walizozipata ni kuwa magari yote yaliendelea na safari zake baada ya tukio hilo.

“Inasemekana basi la Moro Best liliendelea na safari yake na Lowassa naye aliendelea na safari yake ila vioo tulivyovikuta hatujajua ni vya gari gani,” alisema Gindo.

Kuhusu harambee

Katika harambee hiyo, Lowassa alifanikiwa kuchangisha zaidi ya Sh48 milioni, fedha ambayo ndiyo waliyopanga kuikusanya.

Lowassa alisema yeye na marafiki zake, wanatoa kiasi cha Sh18 milioni ili kuweza kufanikisha shughuli za kanisa hilo.

Alisema anaona faraja kutumia kiasi kikubwa cha fedha zake makanisani na angependa wanaohoji mkakati wake huo kuelewa hivyo.

“Watu wanahoji kwa nini natumia fedha zangu kwenye makanisa, mimi nina Mungu na ninapata faraja kufanya hivi,” alisema Lowassa na kuongeza; Ninachofanya ni kazi ya Mungu.”

Lowassa amekuwa akishiriki katika harambee za ujenzi na shughuli  mbalimbali za makanisa nchini tangu alipokuwa Waziri Mkuu.

No comments:

Post a Comment