Washukiwa wa ubakaji wanafikishwa mahakamani leo
Kesi inayowahusu wanaume watano wanaoshukiwa kumbaka msichana mmoja mwenye umri wa miaka 23 na kisha kumuua nchini India itaanza kusikilizwa leo mjini Delhi.
Mshukiwa wa sita anayemainika kuwa na umri wa miaka 17, anatarajiwa kufikishwa katika mahakama ya watoto.
Kesi hiyo iliwashangaza wengi sana nchini India na kuzua mjadala kuhusu jamii inavyowachukulia wanawake. Wakipatikana na hatia , huenda wakanyongwa.
Wakili wa mmoja wa washukiwa alisema kuwa anapanga kuiomba mahakama ya juu zaidi kuhamisha kesi hiyo nje ya mji wa Delhi.
Wakili huyo, VK Anand, anasema kuwa hamu ya vyombo vya habari kufuatilia kesi hiyo kwa karibu huenda ikasababisha hukumu isiyo ya haki.
''Tuna uhakika hatutapata haki katika kesi hii, ikiwa itasikilizwa mjini Delhi," alisema.
Mbali na hayo, mamake mwathiriwa amelaani matamshi ya baadhi ya watu kuwa mwanawe ndiye alisababisha jambo lililomkumba.
Aliambia BBC kuwa wanasiasa waliotoa matamshi kama hayo, ni wabaguzi wa kijinsia na vile vile hawana maadili na kuwa ni baadhi ya wale wanaounga mkono vitendo kama hivyo.
'Ushahidi wa kina'
Kitendo cha unyama kilichofanyiwa mwanamke huyo, kimesababisha ghadhabu na maandamano kote nchini kuhusu jamii inavyowatendea wanawake, India na serikali imesema kuwa itaweka sheria kali kuhusu dhulma dhidi ya wanawake
Pia imeahidi kuendesha kwa haraka kesi za ubakaji katika siku za usoni. Baadhi ya kesi nchini India huchukua miaka mingi kukamilika.
Kitendo hicho kilizua ghadhabu kote nchini India
No comments:
Post a Comment