Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa
WAKATI Spika wa Bunge, Anne Makinda akitangaza
kufutwa kwa hoja zote binafsi za wabunge kutokana na vurugu zilizotokea
bungeni juzi na jana, Chadema kimewataka wabunge wao wasiende kwenye
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge hadi pale rufaa zao 10
zitakapotolewa uamuzi.
Rufaa hizo ni pamoja na ile ya Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu kulitaka Bunge lisitishe uamuzi wa kupewa
ujaji wa Mahakama Kuu, jaji mmoja kwa madai kuwa hana vigezo vya kuwa
na nafasi hiyo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa
alitoa msimamo huo jana baada ya Spika Makinda kueleza bungeni kuwa
Lissu ndiye kinara wa vurugu, huku ikielezwa kuwa Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge itamchukulia hatua za kinidhamu.
Kabla ya Spika Makinda kuahirisha Bunge,
kulitokea mvutano kati yake na Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki,
Joshua Nassari baada ya Makinda kumweleza kuwa hajui kanuni hivyo
atulie.
Hata hivyo, alimruhusu kuzungumza na ndipo
Nassari alipopinga Kamati ya Uongozi ya Bunge kufuta hoja binafsi za
wabunge akieleza ni kinyume cha kanuni za Bunge kufanyika kitu hicho.
Kabla ya Spika Makinda kujibu, Lissu alisimama
na kuomba mwongozo wa Spika akisema; “Mheshimiwa Spika tunataka
utueleze tutaendelea kukata rufaa hadi lini, wakati una rufaa zetu 10
kuanzia mwaka juzi na hujazitolea uamuzi, naomba mwongozo wako
Mheshimiwa Spika,” alisema Lissu na kujibiwa na Spika Makinda kuwa,
“Rufaa hizo zinafanyiwa kazi na zitatolewa uamuzi.”
Makinda aliliahirisha Bunge kwa kile
alichosema kukithiri kwa vitendo vya utovu wa nidhamu ndani ya Bunge
hilo na kufuta hoja binafsi ambazo hutolewa na kuchangiwa baada ya
kipindi cha maswali na majibu.
Makinda alisema: “Waheshimiwa wabunge, tangu
Januari 30, hadi jana (juzi) Februari 4, 2013 tuliamua kuwasilisha
bungeni hoja binafsi za wabunge ambazo ziliahirishwa katika mkutano wa
tisa wa Bunge kwa nia njema ya kujadiliana masuala makubwa ya kitaifa na
kuishauri Serikali nini kifanyike ili kukabiliana na matatizo
mbalimbali yanayowahusu wananchi.
“Hata hivyo, imelazimu kuahirisha mijadala
yote ya hoja binafsi kutokana na tabia iliyojitokeza ya utovu wa nidhamu
kwa baadhi ya wabunge na hivyo kuamua kwa makusudi kuanzisha vurugu na
kulifanya Bunge kupoteza heshima yake,” alisema Spika Makinda.
Alisema kutokana na hali hiyo, Kamati ya
Uongozi imekubaliana kuwa suala hilo lipelekwe kwenye Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge ili ilichunguze na kuwasilisha mapendekezo
yake kabla ya mkutano unaoendelea kumalizika na kwamba hoja zote binafsi
zisiwasilishwe kutokana na utovu wa nidhamu ambao ungeweza kujitokeza
katika hoja zilizobakia.
Hata hivyo, Lissu alisema kuwa kelele za kutetea taratibu na kanuni ndizo zinamfanya aonekane kuwa ana utovu wa nidhamu.
“Spika anaonyesha upendeleo wa waziwazi,
anakiuka kanuni kwa makusudi. Mimi nitasema, sitaogopa kamati, hata
nikiitwa nitasema... Sasa tunachokifanya, tumekutana leo (jana) na
tumeandaa taarifa ya kutaka Spika aondolewe yeye na naibu wake, hii
tutaiwasilisha kama taarifa kati ya kesho (leo) na keshokutwa (kesho),”
alisema Lissu.
Juzi Naibu Spika, Job Ndugai naye aliahirisha kikao cha Bunge
kilichokaa kwa dakika 43 ikiwa ni muda mfupi zaidi baada ya kutokea
vurugu zilizoanzishwa na kambi ya upinzani ikiongozwa na wabunge wa
Chadema waliodai kuwa hawatendewi haki.
Akizungumzia hoja ya Mnyika, Spika Makinda
alisema, “Kulingana na maelezo hayo ya utangulizi, hoja ya Mnyika,
ilikidhi vigezo na alipewa nafasi na akawasilisha hoja yake.
Baada ya
hoja hiyo kuwasilishwa na kwa mujibu wa kanuni ya 53(6) (c), Waziri wa
Maji ambaye ndiye Msemaji wa Serikali kuhusu hoja husika, alipewa nafasi
ya kuwa mchangiaji wa kwanza na kutoa maoni ya shughuli za Serikali.”
Alisema maoni hayo ya Waziri wa Maji yalizingatia Kanuni ya 57(1) (c) inayoruhusu kuingiza au kuongeza maneno mapya kwenye hoja.
Makinda alisema: “Kwa masikitiko makubwa sote
tulishuhudia vurugu zilizojitokeza katika Bunge hili hasa wakati wa
mjadala wa hoja binafsi za wabunge. Kimsingi huu ulikuwa ni utovu wa
nidhamu wa hali ya juu kutokea katika historia ya Bunge letu.”
Dk Slaa amshukia
Akizungumza
hukusu matukio hayo, Dk Slaa alisema amewazuia wabunge wake kuonana na
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kama wakiitwa hadi hapo
rufaa zao 10 zitakazotolewa uamuzi.
“Tumeshawaeleza wabunge wetu
wasiende kwenye kamati hiyo hadi Spika wa Bunge na Naibu wa Spika
watakapotoa uamuzi wa rufaa zetu 10 mbele ya Bunge letu la Jamhuri ya
Muungano,”alisema Dk Slaa.
Dk Slaa alisema wanalaani kitendo cha Spika wa
Bunge, Naibu wa Spika na wenyeviti wa Bunge kwa kitendo cha ubaguzi wa
wazi kwa wabunge wa upinzani, kinyume na Kanuni ya 8 ya Bunge inayotaka
watende haki, uadilifu bila chuki kwa wabunge wote.
Alilaani kitendo cha Naibu Spika Ndugai kuleta
ubaguzi wa kutopitisha hoja binafsi ambazo zingeleta tija kwa wananchi
zilizowasilishwa bungeni na Mnyika.
“Jana ilitokea fujo bungeni hivyo Naibu Spika
alitakiwa asitishe Bunge kwa muda hadi utulivu utakaporejea, lakini
alichokifanya ni kafuta hoja ya Mnyika aliyoiwasilisha bila ya kuwahoji
wabunge. Huu ni ukiukwaji wa kanuni za Bunge zinavyosema,” alisema Dk
Slaa.
Alisema alishangazwa na uongo wa Spika Makinda bungeni akieleza
kuwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe alisimama kwa kifungu 53
(c) wakati alisimama kwa kutumia kifungu 51(c) akipendekeza kuondolewa
bungeni kwa hoja binafsi ya Mnyika.
“Spika amekuwa mpotoshaji, muongo na kumsemea,
Waziri wa Maji amesimama kwa kutumia kanuni ya 53(c) wakati alitumia
kanuni ya 51 (c), kanuni inataka kama hoja imefikishwa bungeni
isiondolewe. Kilichotokea hoja imeondolewa,”alisema Dk Slaa.
Nasari alalama hoja
kuzimwa
Nassari
aliyekuwa awasilishe hoja yake, kuhusu mwenendo wa Baraza la Mtihani la
Taifa unavyoathiri elimu nchini, alisema kuwa atakata rufaa kupinga
uamuzi wa Spika.
“Nitakata rufaa Kamati ya Uongozi, hoja yangu
iliahirishwa mkutano uliopita, halafu leo inaondolewa bila sababu, kweli
sikubali kwa sababu hoja yangu haihusiani na vurugu zilizotokea,”
alisema.
Lukuvi apigilia msumari
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisema: “Kamati ya
Uongozi ndiyo inayopanga shughuli za Bunge na ndiyo inayomshauri Spika
inapoona kuna tatizo kabla, wakati na baada ya Bunge.
“Sasa, imeamriwa hivyo kufuta hoja na iko
katika kanuni...Unajua Kamati ya Uongozi, mimi naingia kwa nafasi yangu
pamoja na Mwanasheria Mkuu,.Sasa hizi hoja binafsi ilikuwa ni ‘favour’
(fadhila) tu sasa tunaona zinakoelekea siko na uamuzi tuliofikia ni
kuziondoa.”
No comments:
Post a Comment