Picha ikionyesha tukio lililofanywa na Mbunge wa Tabora Mjini,Aden Rage.
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime
amesema kuwa wanaandaa jalada la kuhusika kwa Mbunge wa Tabora Mjini,
Ismail Aden Rage kwa ajili ya kuliwasilisha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka
(DPP).
Kamanda Misime alisema jana kuwa wako mbioni
kukamilisha jalada hilo ili walipeleka kwa DPP kwa ajili ya kufikishwa
mahakamani.“Ni kweli tumepokea malalamiko ya Chadema na tunaandaa
malalamiko ili kuwasilisha kwa mwanasheria na Serikali,” alisema Misime.
Hayo
yamekuja kutokana na vurugu zilizotokea kati ya wafuasi wa Chadema na
baadhi ya wabunge wa CCM, akiwamo Rage wakati walipokuwa wakigombea
mlingoti wa bendera kitendo kilichosababisha watu watatu kujeruhiwa
katika tukio hilo wikiendi iliyopita mjini Dodoma.
Hata hivyo, Rage
amekana kuhusika na vurugu hizo akisema anaamini uchunguzi kuhusu tukio
hilo utamuweka huru kabla au baada ya kufikishwa mahakamani kwa sababu
hakushiriki wala kumpiga mwanaChadema aliyetangaza kumshtaki.
“Sikumpiga.
Historia yangu inaonyesha kuwa sijawahi kushiriki vitendo vya vurugu
wala mapigano kwa sababu yoyote ile. Mimi siyo mhuni wa kupiga mtu.
Nilichofanya ni kumlinda yule kijana asipigwe na wanaCCM waliojaa hasira
kwa yeye kuingilia mkutano wetu,” alisema Rage, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba.
Alisema kada wa Chadema ndiye
chanzo cha vurugu hizo zilizoishia kwa kujeruhiwa na wanaCCM baada ya
kuvamia eneo la mkutano wa chama hicho.
“Baada ya kuona kitendo hicho, mimi pamoja na
Mwenyekiti wa CCM wa Iringa, Deo Sanga, kama viongozi tulimfuata kijana
yule na kumsihi asifanye hivyo baada ya kuona vijana wa CCM waliokuwapo
eneo lile wanaanza kupandisha jazba ambazo tusingemudu kuzizuia, lakini
hakutusikilizwa,” alisema.
Rage alisema baada ya kuona kijana
huyo anaanza kushambuliwa na wanaCCM ndipo alipolazimika kuingilia kati
kuwaamulia na kumkinga asipigwe na mawe na majabali yaliyokuwa
yameshikwa na wanaCCM, ambapo kijana huyo alifanikiwa kuchomoka na
kukimbia.
Alisema kabla ya vurugu, kundi dogo la wafuasi wa
Chadema lilikuwapo eneo la mkutano wakiwa na bendera ya chama hicho bila
kufanya vurugu yoyote, ambapo yeye aliwasihi kuwaacha wasikilize sera
za chama hicho kwani mkutano ulikuwa wazi kwa wananchi wote bila kujali
itikadi za vyama.
Hata hivyo, picha zilizopigwa na kuchapishwa
kwenye vyombo vya habari zilimwonyesha Rage na wafuasi wa CCM wengine
wakiwa katikati ya vurugu hizo na juzi uongozi wa Chadema Wilaya ya
Dodoma ulitangaza kumburuta mahakamani mbunge huyo kwa tuhuma za
kujeruhi, kung’oa na kuharibu mali za chama hicho kikuu cha upinzani
nchini.
Kauli ya Rage imetokana na kitendo cha uongozi wa Chadema
wa Wilaya ya Dodoma kutangaza nia ya kumshtaki baada ya kumpiga kada
wao.
Makada wa CCM na Chadema walipigana Jumapili iliyopita wakati wa maadhimisho ya miaka 36 ya CCM mjini Dodoma.
Vurugu
hizo zilizuka baada ya wafuasi wa Chadema kukasirishwa na kitendo cha
vijana wa CCM kung’oa bendera yao wakati wakiendesha mkutano kwenye eneo
la Mwanga Baa mjini Dodoma.
Wafuasi hao wa Chadema walilazimisha
kurudisha bendera yao wakati mkutano ukiendelea, ndipo makada wa CCM
waliojumuisha wabunge wa Jamhuri ya Muungano walipoamua kuwapiga kwa
kuwarushia mawe wafuasi hao na kusababisha kuumia kichwani kwa kada wa
Chadema.
Wabunge wa CCM waliokuwa katika tukio hilo
ukiacha Rage ni pamoja na Seleman Jafo, Said Mtanda, Mary Chatanda na
Nyambari Nyangwine.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumzia
suala hilo alimtetea Rage, akisema alikuwa akiamua ugomvi huo na kama
isingekuwa yeye mauaji yangetokea.
“Hakuhusika yeye alikuwa akiamua ugomvi na kama asingekuwepo mauaji yangetokea,” alisema Ndugai.
Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama alisema kwamba hajapata taarifa za kuwapo kwa tukio hilo.
No comments:
Post a Comment