Deni la taifa; kila Mtanzania anadaiwa Sh450,000
Bendera ya Taifa
Baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza matokeo
ya sensa, inayokaribia watu 45 milioni, siku chache baadaye deni la
taifa lilitangazwa kufikia Sh21 trilioni huku katika wastani kila mtu
akidaiwa Sh467,404.
Fedha hizo zinatokana na mkopo baada ya
Serikali kukopa kwa ajili ya kujenga miundombinu kama barabara, bomba la
gesi, mishahara ya wafanyakazi, na miradi mingine.
Kwa mujibu wa
taasisi isiokuwa ya kiserikali ya Tanzania Coalition on Debt and
Development (TCDD), serikali inadaiwa ‘mzigo wa madeni’ unaofika Sh21
trilioni.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo Hebroni Mwakagenda,
anafafanua kwamba Serikali inakopa fedha hizo Benki Kuu (BoT), Benki za
Biashara, Kampuni za Bima na Mashirika ya Hifadhi za Jamii, Benki ya
Dunia (WB), Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) na Shirika la Fedha
Ulimwenguni (IMF).
Mwakagenda anasema deni limeongezeka kwa dola
456.1 milioni sawa na Sh7.3 trilioni katika kipindi cha mwaka mmoja tu,
tangu Oktoba 2011.
Akichanganua kuhusu deni hilo Mwakagenda
abainisha kuwa mpaka kufikia Oktoba mwaka jana, deni la nje lilikuwa
Sh15.9 trilioni, kiwango ambacho ni cha juu kabisa kwa nchi kukopa
kutoka kwenye masoko ya kimataifa. Amesema taarifa za BoT zinaonyesha
kuwa deni la ndani limefikia Sh5.1 trilioni hadi kufikia Oktoba mwaka
jana na kwamba kiasi hicho ni sawa na ongezeko la Sh513 bilioni tangu
mwaka 2011.
“Deni la ndani linakua kwa kasi kubwa kwa sababu
Serikali imeanza kukopa kwenye benki za biashara ambazo zinatoza riba
kubwa. Hii ni hatari kwa uchumi wa nchi,” anasema Mwakagenda.
Vizazi vijavyo kulipa deni
Dk
Prosper Ngowi, kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro anasema deni siyo
kitu kibaya ila tatizo likuja endapo fedha zilizokopwa zimetumika
vibaya.
“Deni hili ni kubwa na hali ni mbaya kwa kuwa litalipwa
na riba na haliwezi kumalizika leo litaendelea hadi kizazi kijacho,”
amesema Dk Ngowi.
Kwa upande wake Profesa Humfrey Moshi wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, anasema ni lazima tujiulize deni hilo linatokana na
miradi gani.
“Tuangalie fursa za kukopa na tupunguze matumizi
yasiyokuwa ya lazima kama magari ya kifahari, safari zisizokuwa za
lazima, kuwa na wajumbe wengi katika mambo madogo,” ameshauri Profesa
Moshi.
Wakati wataalamu hao wakizungumza hivyo, takwimu za Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais,Mahusiano na Uratibu Stephen Wasira,
alipowasilisha bungeni taarifa ya hali ya uchumi kwa mwaka 2011 na
mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2012/13— zilionyesha kwamba pato
la Taifa lilikuwa kwa Sh37.5 trilioni.
Hii inatokana na idadi ya
watu Tanzania Bara, ambao wanakadiriwa kufikia 43.2 milioni mwaka 2010
na watu milioni 44.5 mwaka 2011, na pato la wastani la kila mtu lilikuwa
Sh869,436.3 mwaka 2011. Mbali na hayo ukuaji halisi wa pato la Taifa
ulikuwa kwa asilimia 6.4 mwaka 2011 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka
2010.
Hivi sasa idadi ya watu inaongezeka kwa asilimia 2.6 kwa
mwaka, kwa kipindi cha mika kumi iliyopita Watanzania milioni 10
waliongezeka.
Rais Jakaya Kikwete anasema idadi ya watu inakuwa kwa kiwango kikubwa na kwamba ongezeko lijalo litakuwa mzigo mkubwa kwa Taifa.
Kwa
mujibu wa Rais kama ongezeko hilo litaendelea, ifikapo mwaka 2016,
Tanzania itakuwa na watu 51 milioni kiwango kisichokidhi mahitaji halisi
ya uchumi na mipango mengine.
Ongezeko hilo lisiloendana na kiwango
cha uzalishaji linatia shaka zaidi huku msongomano wa watu katika miji
mikubwa ukiendelea kuwa mkubwa, kwa mfano Dar es Salaam ina watu 2, 294
kwa kilometa moja ya mraba, ikifuatiwa na Mwanza watu 186 na Kilimanjaro
126.
Wasiwasi wa Rais unakuja huku Waziri wa Kazi na Ajira,
Gaudentia Kabaka akitoa ripoti mwezi machi mwaka jana kwamba kiwango cha
ukosefu wa ajira nchini ni asilimia 11.7 kwa watu wenye umri wa kuanzia
miaka 15 na kuendelea.
Wasira anasema vijana walioajiriwa wenye
umri wa miaka 15 hadi 34 ni milioni 9.5 sawa na asilimia 86.6 na vijana
wasio na ajira ni milioni1.4 sawa na asilimia 13.4 ya nguvukazi yote ya
taifa.
Mbali na hayo Dk Ngowi anasema watu 1.6 milioni tu ndiyo
wanaolipa kodi, na wengine wasiolipa huku idadi kubwa iliyobaki ikiacha
mzigo huo kwa watu wachache.
Dk Ngowi anasema ili kujinasua na
janga hilo, serikali inatakiwa kukusanya mapato ya kutosha ya ndani,
lakini pia ijiepushe na matumizi yasiyokuwa ya lazima.
Kuhusu elimu
kutolewa bure, Dk Ngowi anasema mpango huo unatia shaka kwa kuwa
Tanzania nchi maskini hivyo huduma za elimu bure, itakuwa na uwalakini.
Anabainisha kwamba ni bora elimu iwe ya kulipia, lakini iwe ya kiwango kinachotakiwa.
Serikali ikope kwa nidhamu
Naye
Profesa Moshi alitahadharisha kuwa kama nchi itaendelea kuwa na madeni
makubwa kiasi hicho, basi itashindwa kupiga hatua katika maendeleo yake
ya kiuchumi kwa miaka ijayo.
“Nchi inapokuwa na deni kubwa kama hili,
inaweza kuzuia wawekezaji wasije, kwa sababu watalazimishwa kulipa kodi
kubwa ili kupunguza deni la nchi. “Tukope endapo kuna suala la muhini
na ni lazima kufanya hivyo,” anasema Profesa
Kauli za wataalamu
hao wa uchumi zinaoana na ile ya Mwakagenda ambaye pia anasema serikali
inapaswa kufikiri mara mbili kabla ya kuamua kukopa, na kuwapo kwa
nidhamu katika kukopa kwa kuwa deni hilo limevuka kiwango cha kimataifa.
Katika
mapendekezo yake Mwakagenda anasema umefikia wakati kwa Serikali
iruhusiwe kukopa baada ya ya Bunge kujadili kwa sababu mikopo mingi
haina faida zaidi ya kuwaumiza wananchi.
Profesa Moshi
anatahadharisha serikali isije kuomba kufutiwa madeni kama mwaka 2000
kupitia Mpango wa Nchi Maskini zenye Madeni Makubwa (HIPC).
Wakati
deni hilo likiwa kubwa kiasi hicho, malengo ya uchumi na mendeleo ya
jamii kwa Serikali katika mwaka 2012/13 ni pato la taifa kukua kutoka
asilimia 6.8 na kufikia asilimia 8.5 mwaka 2016.
No comments:
Post a Comment