Rais Jakaya Kikwete, leo anatarajia kuzindua
mfumo wa Taifa wa Usajili na Utambuzi wa Watu na kutoa vitambulisho vya
Taifa katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
na gazeti hili jana, , Ofisa Habari wa Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa (Nida), Rose Mdami alisema maandalizi ya uzinduzi huo yamekamilika
na kwamba utahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa
wakiwamo mabalozi na mawaziri wakuu wastaafu.
Alisema katika
uzinduzi huo, Rais Kikwete na baadhi ya viongozi wakuu wa kitaifa
watapatiwa vitambulisho vyao vya taifa na baadaye vitambulisho hivyo
vitatolewa kwa watu wote waliosajiliwa na kuchukuliwa alama za vidole.
Aliongeza
kuwa picha na saini za kielektroniki zimechukuliwa na kwamba zoezi hilo
litaanzia kwa wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na watumishi wa
umma ambao taarifa zao zimekwishachukuliwa. “Maandalizi yote ya sherehe
yamekamilika na kwamba baada ya uzinduzi huu kinachofuata ni kuwapatia
vitambulisho watumishi wa umma na wengine ambao taarifa zao
zimeshachukiliwa,” alisema Mdami.
Aliongeza kuwa baada ya makundi
hayo maalumu watafuatia wananchi wa kawaida kwa awamu ambao
watachukuliwa alama za vidole, picha na saini za kielektroniki na
hatimaye kuwapatia vitambulisho hivyo.
Kwa mujibu wa Mdami,
uzinduzi huo unafanyika baada ya kukamilika kwa hatua mbalimbali ikiwamo
ununuzi na upokeaji wa baadhi ya vifaa vya usajili ambavyo ni muhimu na
msingi wa ujenzi wa mfumo wa usajili na utambuzi wa watu.
No comments:
Post a Comment