Biashara kuuza mabinti yashika kasi

  Wazazi wapokea kati ya Sh. 200,000 hadi 500,000/-
  Wapya na wakala wao wanaswa Bandari D�Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Kapteni Mstaafu Chiku Gallawa

Wakati biashara ya kuuza wasichana kwenda kutumikishwa ughaibuni ikizidi kushika kasi kwa kukamatwa kwa mabinti wengine wapya saba na wakala wao Bandarini Dar es Salaam, uchunguzi huru wa NIPASHE wilayani Lushoto umegundua kuwa tamaa ya fedha za bila jasho na hali ya kukata tamaa ya maisha ndivyo vitu vinachangia udhalilishaji huo.

Nipashe imethibitishiwa wilayani Lushoto kuwa baadhi ya wazazi hufikia hatua ya kuuza watoto wao kati ya Sh. 200,000 na 500,000 kwenda kutumikishwa ughaibuni katika biashara ya binadamu ambayo imeshika kasi nchini.

Wengi wa watoto wanaohusishwa katika biashara hiyo haramu ni wasichana wenye umri wa kati ya miaka minane hadi 15.

Hayo yakiendela Lushoto, jijini Dar es Salaam, kati ya Jumamosi iliyopita na jana walikamatwa mabinti saba, vyanzo vya polisi wa maji vimethibitisha.

Waliokamatwa Jumamosi na Jumapili wiki iliyopita, ni mabinti watatu wakitokea Mtwara, Ruvuma na Pwani. Wote walikamatwa katika bandari ya Dar es Salaam.

Mabinti hao ni mwenye umri wa miaka 13 kutoka wilaya ya Masasi mkoani Mtwara; mwenye miaka 12 kutoka Tunduru (Ruvuma) na mwenye miaka 13 kutoka Kisarawe (Pwani).

Bila kujali habari ambazo zimekuwa zikitolewa juu ya kukamatwa kwa wasichana wengine na mawakala wao katika biashara hii haramu ambayo inavunja utu wa watu kinyume cha Sheria namba sita ya mwaka 2008 ya kupinga biashara ya binadamu (The Anti Trafficking in Persons Act no. 6 of 2008), Jumatatu wiki hii mabinti wengine wawili walikamatwa.

Mmoja mwenye miaka 10 kutoka Ruvuma na mwingine mwenye miaka 13 kutoka Lindi.

Jana mabinti wengine wawili na wakala mmoja walikamatwa. Mabinti hao ni kutoka Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi,  mmoja ana miaka 16 na mwingine miaka 15.

Nipashe ilifuatilia wanakotoka watoto hao na katika uchunguzi wake wilayani Lushoto imethibitisha kuwa biashara hiyo imeshika kasi katika baadhi ya vijiji vya wilaya ya Lushoto, ambako baadhi ya wazazi wamekuwa walipwa fedha hizo na mawakala wanaofanya kazi hiyo ili kukubali watoto wao wasafirishwe kwenda nje ya nchi kufanya kazi mbalimbali zikiwamo za ndani.

Kushamiri kwa biashara hiyo vijijini kumebainika baada ya NIPASHE kufika katika kijiji cha Manolo kata ya Mtae tarafa ya Mlalo wilayani hapa kufuatilia taarifa za mtoto mmoja (jina tunalo) mwenye umri wa miaka 14 aliyekamatwa Januari 25, mwaka huu katika Bandari ya Dar es Salaam akitokea kijiji hicho akisafirishwa kwenda nchi za Uarabuni.

MWENYEKITI WA KIJIJI

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Manolo, Ombeni Praygod, akizungumza na NIPASHE katika ofisi ya kijiji akiwa na Ofisa Mtendaji wa kijiji, Athumani Mkande, alithibitisha kuwa mtoto huyo anatoka kitongoji cha Luguruwa kilichopo katika kijiji hicho na kwamba hafahamu kama alikuwa amemaliza darasa la saba au la.

Katika uchunguzi zaidi majirani wa nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo, walisema baada ya taarifa za kuuzwa watoto kuanza kutolewa katika vyombo vya habari, wazazi  wa mtoto huyo aliyekamatwa jijini Dar es Salaam wameondoka kijijini hapo kuhofia kuchukuliwa hatua za kisheria.

JIRANI

Mmoja wa majirani hao, Ally Ibrahimu, alisema siyo mara ya kwanza kwa wazazi kutoka kitongoji hicho kuruhusu watoto wao kwenda kufanya kazi nje baada ya kuombwa na watu.

“Hili ni jambo la kawaida mzazi kuamua mtoto wake apelekwe nje ya nchi, kwanza anakuwa amepunguziwa gharama za maisha kwa sababu kumhudumia mtoto hasa mwanafunzi ni gharama kubwa kutokana na hali ya maisha ilivyo ngumu kwa sasa,” alisema Ibrahimu.     

Uchunguzi uliofanywa kwenye vijiji cha Humboyo, Mrifu, Madala na Manolo, umebaini kuwa biashara ya binadamu imeendelea kufanyika kwenye vijiji hivyo na watoto wanasafirishwa kwenda nje kupitia mpaka wa Namanga uliopo mkoani Arusha.

Imebainika kuwa wazazi wanalazimika kukubali watoto wao kuchukuliwa kwa kushawishiwa kupewa pesa na kuahidiwa kujengewa nyumba za ibada na wafadhili waliopo nchini za Uarabuni ambao huwachukua watoto hao.

Uamuzi wa wazazi kukubali watoto wao wachukuliwe kwenda nje hata kama hawafahamu wanakwenda kufanya kazi gani, unatokana na hali ngumu ya maisha na hivyo mawakala wanapokwenda kuwapa pesa wanakubali.

Taarifa zaidi za kiuchunguzi zimebaini kuwa katika mkoa wa Tanga, siyo wilaya ya Lushoto tu ambayo baadhi ya wazazi wanakubali watoto wao kuchukuliwa kwenda nje kufanya kazi za ndani, bali tatizo hilo lipo pia katika wilaya za Handeni na Kilindi.

Kutokana na tatizo hilo, watoto wanaochukuliwa baadhi yao wanakuwa hata hawajamaliza elimu ya msingi hali ambayo imekuwa ikisababisha kuzorota kwa kiwango cha elimu katika baadhi ya wilaya za mkoa huo.

RC TANGA

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Kapteni Mstaafu Chiku Gallawa, akizungumzia suala hilo, alisema kufanya kazi za ndani katika nchi za Urabuni hususani Oman ni halali na kwamba hata Balozi wa Tanzania nchini humo anawapokea watu wanaokwenda kufanya kazi za ndani.

Hata hivyo, Gallawa alisema kama wapo baadhi ya wazazi ambao wanaruhusu watoto wao kwenda nje kufanya kazi za ndani wakiwa na umri chini ya miaka 18 ni kosa ambalo serikali ikiwabaini, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Wazazi wasikwepe majukumu yao, watoto wenye umri chini ya miaka 18 wanatakiwa kuwa chini ya uangalizi wao na siyo kuruhusu waende nje ya nchi kufanya kazi za ndani, tutafanya uchunguzi kuwabaini wazazi wenye tabia hiyo,” alisema Gallawa. 

OFISA MTENDAJI

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Manolo, Athuman Mkande, akizungumza katika mahojiano na NIPASHE kijijini kwake, alisema biashara ya watoto ipo na wanaochukuliwa miongoni mwao wamo watoto wa shule za msingi na sekondari ingawa inafanyika kwa usiri mkubwa.

Mkande alisema ujanja unaotumiwa na mawakala wanaofanya biashara hiyo, ni kwamba wakifika katika kijiji husika, wanamtafuta mwenyeji wao ambaye ndiye anafanya kazi ya kushawishi wazazi wa mtoto wakubali kumruhusu kwa kumueleza kuwa wanakwenda kumtafutia kazi ambayo itakuwa na manufaa kwa familia.

Alisema kutokana na kushamiri kwa tatizo hilo, serikali ya kijiji inapobaini mwanafunzi fulani hajafika shuleni kwa muda mrefu, taarifa zinatolewa kwa kumwita mzazi ahakikishe anamtafuta mtoto alipo ili aendelee na masomo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Manolo Praygod, alisema baadhi ya watoto wamekuwa wakitoroka bila hata kuwaaga wazazi wao kutokana na kushawishiwa na mawakala baada ya kupewa vizawadi vidogo vidogo.

Praygod alisema mawakala huwatumia zaidi kina mama ambao muda mwingi wanakuwa na watoto kwa kukubaliana kinyemela bila baba zao kujulishwa, lakini baba akibaini mtoto haonekani huelezwa kuwa amepelekwa kwa ndugu wa upande wa mwanamke.

Aliongeza kuwa wanaowatorosha watoto hao wanafanya kazi hiyo kwa usiri mkubwa sana na wakishakubaliana na wazazi, fedha wanazokuwa wamekubaliana hulipwa nusu na nyingine hutumiwa kwa njia ya mtandao wa simu.

“Kimsingi, yapo manufaa ambayo baadhi ya wazazi wanayapata kwa watoto wao kuchukuliwa kwenda nje kufanya kazi ambazo nyingine hazijulikani kwa mfano, kuna ndugu yetu mmoja (analitaja jina) alijengewa msikiti baada mtoto aliyechukuliwa kwenda Uarabuni,” alisema Praygod.

DC LUSHOTO

Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Majid Mwanga, alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, alisema ni jipya kulisikia kutokea katika wilaya yake na kuahidi kufutilia kwa kina ili serikali ichukue hatua.

“Hili ni suala geni katika wilaya yangu kulisikia, lakini kwa sababu kazi ya vyombo vya habari ni kuibua mambo, nitalifanyia uchunguzi na kutoa taarifa, lakini kwa sasa siwezi kueleza chochote kwa sababu ni suala la kiuchunguzi,” alisema Mwanga.

Uchunguzi ambao umeendelea kufanywa na NIPASHE umebaini kuwa watoto wanaonunuliwa na mawakala kutoka mikoani wakifikishwa Dar es Salaam kabla ya kupelekwa Zanzibar mawakala wanawatafutia barua kutoka kwa wenyeviti hao ili wasisumbuliwe bandarini kwa kuwa hawana vitambulisho.

Uchunguzi huo umebaini kuwa biashara hiyo iliibuka kuanzia Desemba mwaka jana na kushika kasi Januari mwaka huu na wanaosafirishwa wengi ni watoto wa kike kutoka mikoa mbalimbali nchini. Wapo wachache wa kiume pia.

 Uchunguzi huo ulibaini kuwa mikoa ambayo watoto hao wananunuliwa ni Mtwara, Lindi, Manyara, Pwani, Tabora, Ruvuma, Tanga na Shinyanga.

Taarifa zinaonyesha kuwa mawakala hao wakishafanikiwa kuwapata watoto hao kutoka katika mikoa hiyo huwapeleka jijini Dar es Salaam na baadaye kusafirishwa kwa usafiri wa majini kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Zanzibar.

Watoto hao wakifikishwa Zanzibar hukutana na watu maalum ambao huwapokea na kufawanyia mipango ya kuwasafirisha kwa usafiri wa ndege au wa majini kwenda Uarabuni ambako hutumikishwa kazi mbalimbali.

Mawakala hao wakifanikiwa kuwasafirisha kutoka Bandari ya Dar es Salaam hulipwa wastani wa Dola za Marekani 5,000 (Sh. milioni 8) kwa kila mtoto wanayefanikisha kumvusha kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar.

Kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita wastani wa watoto kati ya watano hadi 10 hufika katika Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusafiri kwenda Zanzibar kila siku.

NIPASHE ina taarifa za kina za watoto wenye umri kati ya miaka minane na 15 kutoka kijiji cha Nakapanya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma;  mkoa wa Tabora; kutoka kijiji cha Mkangula Mkoa wa Mtwara na kijiji cha Mbembaleo pia cha mkoani Mtwara.

Pia wamo kutoka kijiji cha Manoro Wilaya ya Lushoto Mkoa wa Tanga; kutoka Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma; kutoka kijiji cha Namalumbusi Wilaya ya Masasi Mkoa wa Mtwara na kutoka Mkoa wa Manyara.

Wengine waliokwisha kukamatwa wanatoka kijiji cha Ndanda Mkoa wa Mtwara; kijiji cha Mteruka wilayani Nachingwea Mkoa wa Lindi na kutoka kijiji cha Mnazi mmoja Mkoa wa Mtwara.

Wapo pia kutoka kijiji cha Mnazi Mmoja mkoani Mtwara, kutoka kijiji cha Kokoro wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga na mwingine mkazi wa Manispaa ya Iringa mkoani Iringa.

Wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Maji, Mboje Kanga, aliliambia NIPASHE kuwa mawakala watano walikamatwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na sakata hilo.

Alisema kuwa mawakala waliokamatwa ni wakazi wa Zanzibar na kwamba hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa dhidi yao.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment