Maandamano Tunisia baada ya mauaji

Maandamano makubwa ya upinzani yamezuka nchini Tunisia baada ya mauaji ya mwanasiasa wa upinzani.

Shokri Belaid (pron: Belaeed) aliuawa kwa kupigwa risasi likiwa tukio la kwanza tangu mapinduzi ya kiraia mwaka 2011.

Alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali.

Maelfu ya waandamanaji mjini Tunis na Sidi Bouzid --ambako maandamano yalianzia, wamelaumu chama tawala cha Ennahda kwa mauaji hayo.

Polisi wamelazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kujaribu kuwatawanya.

Kiongozi wa chama tawala, Rached Gannouchi,amelaani vikali mauaji hayo akisema kuwa waliomuua walikuwa na nia ya kuanzisha ghasia.

Shrokri Belaeed wa chama cha (Unified Democratic Patriot Party) alipigwa risasi shingoni na kichwani.

Nduguye alithibitisha kuwa bwana Belaid aliyekuwa mratibu wa chama cha Democratic Patriots alifariki baadaye.

Tunisia inakumbwa na mzozo wa kisiasa huku mazungumzo kuhusu mabadiliko katika baraza la mawaziri yakisubiriwa.

Inaarifiwa vyama vingi huenda vikajumuishwa katika muundo wa baraza la mawaziri kwenye serikali ya Muungano inayoongozwa na chama , ingawa mazungumzo kuhusu hili yamekumbwa na hali ya ati ati.

'uhalifu mkubwa'

"Ndugu yangu aliuawa . Nina huzuni mkubwa,'' nduguye marehemu, Abdelmajid Belaid aliambia shirika la habari la AFP .

Haijulikani nani aliyehusika na mauaji hayo.

Duru zinasema kuwa bwana Belaid alikuwa mpinzani mkuu wa serikali iliyoingia mamlakani baada ya mapinduzi ya kiraia mwezi Oktoba mwaka 2011.

Siku ya Jumamosi, aliwatuhumu mamluki waliokodiwa na chama cha Ennahda kwa kuvamia mkutano wa chama chake.

Msemaji wa serikali, Samir Dilou alitaja mauaji hayo kama uhalifu mkubwa .

Nao wanasiasa wa upinzani waliitaja siku ya mauaji kama siku ya huzuni mkubwa Tunisia.

No comments:

Post a Comment