Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai
BAADHI ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wanaoendelea na kikao cha 10, wameulalamikia uongozi wa Bunge
kwa kutojali kufanya marekebisho ya jengo la Bunge wakidai kuwa linavuja
kwa muda mrefu sasa.
Malalamiko ya wabunge hao yalifikishwa kwa Naibu
Spika wa Bunge, Job Ndugai jana, ambapo walisema kwamba wana wasiwasi na
usalama wa jengo hilo.
Ubovu huo ulibainika juzi Ijumaa baada ya mvua
kuanza kunyesha usiku saa saba na kuendelea hadi mchana katika maeneo
mbalimbali ya mji wa Dodoma.
Mbali na eneo linalokaliwa na wabunge kuvuja, maeneo mbalimbali ya jengo la bunge yalikuwa yanavuja.
“Taarifa mheshimiwa Naibu Spika, hili jengo
linavuja, kwa kweli hata hapa nilipokaa ndiyo hasa maji yanapita... sasa
tuhakikishiwe usalama wetu Naibu Spika,” alisema Mchungaji Peter
Msigwa.
Akijibu hoja hiyo, Ndugai alisema, “Taarifa zimefika kwa sasa
wataalamu wetu wa maeneo mbalimbali ya jengo wanafanya kazi kuhakikisha
wanarekebisha hali hiyo.”
Jengo la Bunge mjini Dodoma lililojengwa kisasa
zaidi kwa ushirikiano kati ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa gharama ya
zaidi ya Sh29.8 bilioni kwa sasa lina uwezo wa kubeba wabunge 350 kwa
pamoja, wageni maalumu zaidi ya 100 na wananchi wasikilizaji 200.
Ukumbi huo wa kisasa umekuwa mfano wa kuigwa
ambapo wawakilishi wa mabunge kadhaa kutoka nchi mbalimbali za Afrika
ambao wamekuwa wakifika mjini Dodoma wamekuwa wakiuchukulia kama mfano.
No comments:
Post a Comment