WATU watano wamefariki dunia mkoani Mbeya kwa kupigwa radi
katika matukio matatu tofauti likiwemo lililoua ndugu watatu wa familia moja.
Wanandugu hao watatu wakazi wa kata ya Nyimbili wilayani Mbozi wamefikwa na
mauti Februari 5 mwaka huu majira ya saa saba mchana wakati mvua kubwa
iliyoambatana na radi za mara kwa mara ikiendelea kunyesha wakiwa nyumbani.
Afisa mtendaji wa kata ya Nyimbili Lingtone Nzowa amewataja waliopoteza maisha
kuwa ni Jerumana Halinga(35),David Halinga(5) na Kumi Halinga(3) ambapo pia
radi hiyo imemjeruhi mtoto wa miezi tisa ambaye jina lake halikufahamika mara
moja. Tukio la pili limetokea katika kijiji cha Magurula kata ya Utengule
Usangu Wilayani Mbarali ambapo radi iliyotokana na mvua kubwa imempiga Kasim
Sagutangu na kusababisha kifo chake ambapo diwani wa kata hiyo Juntwa Mwalyaje
amesema mvua hiyo imenyesha Februari 3 majira ya saa nane za mchana. Tukio la
tatu limetokea februari 3 katika kijiji cha Mbagala Kata ya Ilembo wilayani
Mbeya ambapo mwanamke Kotanida Petro amefariki dunia baada ya kupigwa na radi
akiwa shambani kwake. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani
amethibitisha kutokea kwa matukio hayo ya vifo vya watu watano vilivyotokana na
radi.
|
No comments:
Post a Comment