Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), Ludovick Utouh amesema uchunguzi alioufanya dhidi ya vigogo
watatu wa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), unaonyesha kuwa kuna
madudu ya kutisha.
Utouh alisema hivi karibuni kuwa alijikita
zaidi katika mikataba yenye thamani ya zaidi ya Sh500 milioni
iliyoingiwa na shirika hilo.
Awali, Ofisi ya CAG ilitoa ripoti ambayo
ilisababisha aliyekuwa Mkurugenzi wa Tanesco, William Mhando
kusimamishwa na baadaye kufukuzwa.
Vigogo wengine waliotajwa katika ripoti hiyo,
Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja
Mwandamizi Ununuzi, Harun Mattambo walisimamishwa kazi ili kupisha
uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kuingia mikataba
mibovu wakati wa ununuzi wa mali za shirika.
Utouh alisema ripoti hiyo imejaa madudu, jambo ambalo lilisababisha kutumia nguvu kubwa wakati wa ukusanyaji wa taarifa zake.
Alisema baada ya kugundua madudu hayo,
walilazimika kuzunguka kwenye ofisi za shirika hilo zilizoko mikoani ili
waweze kuhoji baadhi ya wafanyakazi na kukagua mikataba hiyo.
Alisema
kutokana na hali hiyo, walitumia nguvu kubwa wakati wa ukusanyaji wa
taarifa zake, jambo ambao lilisababisha kuchukua muda wa miezi mitatu
ili kukamilisha.
“Tumefanya kazi kubwa sana katika ripoti hii
ya awamu ya pili. Hii inatokana na kutakiwa kukagua mikataba iliyoingiwa
na Tanesco ya miradi mikubwa, jambo ambalo lilisababisha kwenda hadi
kwenye ofisi za mikoa ili kuhoji na kuchunguza mikataba hiyo,” alisema
Utouh.
Alisema baada ya kubaini madudu hayo walitoa
mapendekezo yao ambayo Serikali inapaswa kuyafanyia kazi ili waweze
kutenda haki pindi wanapotoa uamuzi kuhusu tuhuma zinazowakabili
viongozi hao.
Alisema kutokana na hali hiyo wamekabidhi
ripoti hiyo tangu Januari mwaka huu kwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo,
Jenerali Robert Mboma ili aipitie na kuiwasilisha kwenye mamlaka
nyingine husika.
Mboma alikiri kupokea ripoti hiyo na kudai kuwa wanaanza kuwahoji watuhumiwa hao wiki jayo.
No comments:
Post a Comment