Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Willfred Lwakatare (wapili
kulia) na Ludovick Rwezahura (kulia) wakiondolewa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu na askari kuelekea kupanda gari kwa ajili ya
kurudishwa rumande, Dar es Salaam, jana.
Dar es Salaam. Mkuu wa Usalama wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare na mwenzake
Ludovick Rwezaura wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
waki kabiliwa na mashtaka manne likiwamo la kula njama ya kutenda kosa
la jinai la kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru Mhariri Mtendaji wa Gazeti la
Mwananchi, Dennis Msacky.
Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu
Mkazi, Emilius Mchauru, Wakili wa Serikali Mkuu, Prudence Rweyongeza
kuwa washtakiwa hao walifanya kosa la kula njama na kutenda makosa ya
jinai kinyume na kifungu cha 384 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya
16 iliyofanyiwa marekebisho 2002.
Rweyongeza alidai kuwa Desemba 28, mwaka jana
katika eneo la King’ong’o katika wilaya ya Kinondoni, washtakiwa hao kwa
pamoja walikula njama kwa kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru Msacky,
kinyume na kifungu cha 227 cha sheria ya kanuni ya adhabu.
Wakili huyo wa Serikali katika shtaka la pili
alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kufanya kosa la
jinai kinyume na kifungu cha sheria cha 24 (2) cha Sheria dhidi ya
Ugaidi, sura ya 21 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Alidai kuwa washtakiwa hao, Desemba 28, 2012
walishirikiana kupanga njama za utekaji nyara dhidi ya Msacky kinyume na
kifungu cha 21 cha sheria inayopinga ugaidi.
Katika shtaka la tatu,
washtakiwa hao wanadaiwa kufanya mkutano wa vitendo vya kigaidi, kinyume
na kifungu cha 5 (a) cha sheria namba 21 inayopinga ugaidi iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Aliendelea kudai kuwa siku hiyo ya tukio,
washtakiwa hao walipanga na kushiriki katika mkutano wa kupanga kitendo
cha ugaidi cha utekaji nyara dhidi ya Msacky.
Kwa mujibu wa shtaka la nne, Lwakatare anadaiwa kuhamasisha vitendo vya ugaidi.
Aliongeza kudai kuwa siku hiyo ya tukio,
Lwakatare akiwa mwenye nyumba, akijua, aliruhusu mkutano kati yake na
Ludovick ufanyike katika nyumba yake kwa lengo la kuhamasisha vitendo
vya kigaidi dhidi ya Msacky.
Baada ya kumaliza kusoma mashtaka hayo,
washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu
Mkazi haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.
“Mheshimiwa Hakimu kesi yoyote inayohusiana na
vitendo vya kigaidi haina dhamana,” alisema Rweyongeza.Rweyongeza pia
aliiomba Mahakama kuruhusu mshtakiwa Ludovick kurudishwa polisi
kuendelea na shughuli za upelelezi.
Lwakatare anatetewa na mawakili, Peter Kibatala, Mabere Marando, Abdallah Safari, Nyaronyo Kichere na Tundu Lisu.
Wakili wa utetezi, Kibatala aliiomba Mahakama
kutoa dhamana kwa mteja wao kulingana na mazingira husika na kwamba
izingatie kuwa dhamana ni haki ya msingi ya mshtakiwa.
“Ugaidi siyo
kosa dogo ni kitu kikubwa iwapo chombo cha kisheria kinachukua haki ya
mtu ya dhamana ni lazima kuwapo na sababu zinazojitosheleza kuwa mtu
huyu kweli ni hatari na Mahakama iridhie kweli ni hatari na anyimwe
dhamana,” aliongeza Kibatala.
Wakili Lissu aliunga mkono hoja za wakili Kibatala.
Kwa
upande wa wakili Safari aliitaka Mahakama ichukue kumbukumbu kuwa
vitendo vya kubambikia kesi watu vimekithiri katika nchi hii.
Hakimu Mchauro atatoa uamuzi kesho Jumatano kama washtakiwa hao watapata dhamana ama la.
No comments:
Post a Comment