Raila Odinga (kushoto) na Uhuru Kenyatta.
14,337, 399: Idadi ya Wakenya waliojiandikisha kupigakura
7,000: Idadi ya waangalizi wa uchaguzi
3,000: Watakaopiga kura nje ya Kenya (Afrika Mashariki)
99,000: Idadi ya polisi watakaosimamia usalama
14: Siku mbazo kesi kuhusu matokeo ya Rais zitasikilizwa na kuamuliwa
WANANCHI wa Kenya leo wanapiga kura kuwachagua
viongozi wao katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza baada ya kupata Katiba Mpya,
ambao unawapambanisha vikali watoto wa waasisi wa taifa hilo ambao sasa
ni marehemu.
Uchaguzi wa leo unaelezwa kuwa na kinyang’anyiro
kikali ambacho hakijawahi kushuhudiwa baina ya wagombea wawili wa urais,
Uhuru Kenyatta wa Muungano wa Jubilee na Raila Odinga wa Cord.
Uhuru ni mtoto wa Rais wa kwanza wa Kenya, Mzee
Jomo Kenyatta wakati Raila ni mtoto wa aliyekuwa makamu wa Kenyatta,
Jaramog Oginga Odinga.
Mbali na wagombea hao wenye matumaini ya kuingia
Ikulu kila mmoja, wapo wengine sita – Musalia Mudavadi (UDF), Peter
Kenneth (Eagle Alliance), Martha Karua (Narc), Mohammed Abduba Dida
(ARK), Prof James ole Kiyiapi (RBK) na Paul Muite wa Safina.
Wagombea wote walihitimisha kampeni zao Jumamosi
na jana hakukuwa na kampeni kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Kenya.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), imesema maandalizi yote
yamekamilika na vifaa vyote vya kupigia kura vimeshafika katika maeneo
husika.
Mwenyekiti wa IEBC, Ahmed Hassan alisema katika
taarifa yake jana kuwa vituo vitafunguliwa saa 12:00 asubuhi na kufungwa
saa 1:00 jioni, lakini kama kutakuwa na wapigakura kwenye foleni
wataendelea hadi watakapokuwa wamemaliza kupiga kura.
Kwa mujibu wa Hassan, kura zote zitahesabiwa vituoni na matokeo kutumwa kwa njia ya simu.
Kwenye kampeni zao za lala salama wagombea wenye
nguvu, Odinga na Kenyatta, wamewahamasisha wapigakura kujitokeza kwa
wingi na kuwachagua, ili waweze kushinda katika raundi ya kwanza.
Msukumo huo unatokana na uwezekano wa kura kupigwa
kwa raundi ya pili Aprili 10, kutokana na uwezekano wa wagombea wote
wanane kushindwa kufikisha nusu ya kura zote, kwa mujibu wa kura za
maoni zilizofanyika awali.
Wakati uchaguzi wa leo umeigharimu Serikali Sh24.9
bilioni (Sh473.1 bilioni za Tanzania), ule wa marudio unakadiriwa
kugharimu Sh11.2 bilioni (sawa na Sh212.8 bilioni).
Asemavyo Uhuru
Mosi, nina
matumaini kuwa kazi niliyofanya mimi na washirika wangu katika Muungano
wa Jubilee, wafanyakazi makini wa chama changu cha TNA na maelfu ya
wafuasi wangu, italipa.
Pili, ninatamani uchaguzi wa amani na matumaini
haya yanazidi hata furaha ya ushindi wa Jubilee. Sitaki tena Kenya
irejee katika matukio ya 2007/8.
Kwa matokeo yoyote yale nitaungana na washirika na washindani
wangu kuwaonyesha Wakenya kuwa kuna umuhimu wa uchaguzi wa amani na
kwamba Kenya yenye amani ni bora kuliko mgombea au chama.
Raila Odinga
Taifa liko katika
ari ya kutaka mabadiliko. Matumaini ni kwamba Wakenya safari hii
wataamua kuchagua mabadiliko. Kenya lazima itazaliwa upya kesho (leo).
Natambua kuwa baadhi ya wafuasi wetu wametishwa na
kutimuliwa kwenye maeneo yao katika baadhi ya mikoa, lakini sina hofu
yoyote, bali ni matumaini kwa kuwa watu wetu na kwa nchi yangu ya Kenya.
Ujumbe wangu kwa miaka mitano iliyopita umekuwa ni
amani. Amani ndiyo ilinifanya kukaa katika Serikali ya Muungano, ambayo
upande mmoja ulitaka kuchukua kila kitu.
Ninaamini Wakenya watanichagua mimi kuwa Rais wao
wa nne. Wanajua tuliyofanya pamoja kwa muda mrefu na mambo ninayoweza
kuwafanyia.
Kinachofuata
Iwapo mgombea
Rais atafikisha zaidi ya nusu ya kura katika uchaguzi wa leo,
atatangazwa mshindi. Ikishindikana, unafanyika uchaguzi wa marudio baina
ya wagombea wawili wa kwanza. Kati yao atakayepata kura nyingi
atatawazwa kukalia Ikulu ya Kenya
Walikotoka
Anayechaguliwa leo
atakuwa Rais wa nne wa Kenya. Marais watatu waliotangulia ni Jomo
Kenyatta, Rais wa Kwanza; Daniel Arap Moi, wa pili na anayeondoka, Mwai
Kibaki.
Wagombea wawili wanaopambana vikali
Uhuru
Kenyatta na Raila Odinga –Hawa ni watoto wa waasisi wa Taifa la Kenya.
Wakati Uhuru ni Mtoto wa Rais wa Kwanza, Mzee Jomo Kenyatta. Odinga ni
mtoto wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Jaramog Odinga Oginga.
No comments:
Post a Comment