Dar es Salaam. Baadhi ya
makandarasi wadogo nchini, wamewatuhumu mameneja wa Wakala wa Barabara
Tanzania (Tanroads) waliokaa muda mrefu vituo vya kazi kuhusika
kuwanyima zabuni.
Hatua hiyo inadaiwa inatokana na mameneja hao kuweka mtandao wa rushwa, kwa wazabuni wakubwa ambao hupewa upendeleo.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa, makandarasi
hao walidai mameneja hao wamekuwa wakihusika kuwanyima zabuni kwa sababu
ya kutotoa rushwa. “Ukiangalia mameneja wenye tatizo hilo wengi wamekaa
kituo kimoja kwa muda mrefu, hivyo wameweka mtandao wa rushwa hutoa
zabuni kwa wakandarasi wakubwa,” alidai mmoja wa makandarasi hao na
kuongeza:
“Kungekuwa na kipindi maalumu cha meneja kukaa
kituo kimoja, hiyo itasaidia kuvunja mtandao wa rushwa. Ukiangalia
wengine wana zaidi ya miaka saba kituoni.” Makandarasi hao walidai kuwa
uozo huo unalindwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale
ambaye ndiye mwenye jukumu la kuwahamisha, lakini tangu ateuliwe hakuna
uhamisho ambao wameufanya.
Hata hivyo, Mfugale alikanusha kufahamu taarifa za
kuwapo kwa vitendo hivyo vya unyanyasaji na rushwa kwa baadhi ya
makandarasi katika mikoa mbalimbali.
“Sina taarifa hizo na kwanza wewe (Mwandishi wa
habari) ndiyo unayeniambia, kama zipo wazilete ofisini siyo kuongelea
pembeni,” alisema Mfugale na kukata simu. Makandarasi hao walidai wakati
wa utawala wa Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Tanroads, Ephraim Mrema
mameneja hao walikuwa wakibadilishwa vituo baada ya muda.
“Uhamisho wa mwisho kwa mameneja hao ulifanyika
mwaka 2007, wamekaa vituoni mpaka wamezoea. Makandarasi wadogo kama sisi
kazi hatupati, wengine wake zao ndiyo walipaji (cashier) wa Tanroads,”
alidai kandarasi mwingine na kuongeza: “Fikiria Mzee (mume) ni meneja,
mama (mke) ni mlipaji halafu wote hawa wanakaa kituo kimoja zaidi ya
miaka nane, nafikiri Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli anatakiwa
kuliangalia hili.”
No comments:
Post a Comment