Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.
Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa amesifia
utawala wake kwa kuongoza taifa bila ya kubaguana na amesikitishwa na
matukio ya udini, ambayo yanaashiria kuvuruga amani na utulivu wa
Tanzania katika siku za karibuni.
Akitoa salamu zake baada ya kusimikwa kwa Askofu
Mpya wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Desdelius Rwoma, Mkapa alisema
anachojivunia ni kuheshimiwa na waumini wa madhehebu yote.
“Katika kipindi cha uongozi wangu, viongozi wa
madhehebu yote walikuwa wakinisisitizia kuwa sisi sote ni ndugu pamoja
na tofauti zetu za kiimani. Wakati wa utawala wangu nilijitahidi kwa
uwezo wangu wote kuwahudumia wananchi bila kuwepo kwa malalamiko ya
kubaguana katika jamii,” alisema Mkapa, ambaye aliiongoza Tanzania
kuanzia mwaka 1995-2005.
Mkapa alionya kuwa taifa limeacha misingi
aliyoiacha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye mara zote
alisimamia umoja wa taifa.
“Wakati wa utawala wangu nilijitahidi kwa uwezo
wangu wote kuwahudumia wananchi bila kuwepo kwa malalamiko ya kubaguana
katika jamii,” alisema.
Mkapa ambaye hakupanga kuongea lolote katika tukio
hilo, alitaka taifa lijenge utamaduni wa kupendana, huku akilaumu kuwa
kizazi kipya cha uongozi kimeanzisha mambo ya ajabu ya kukosa upendo na
kudhalilishana.
Pia alitahadharisha kuwa zama hizi kumeibuka
mitafaruku mbalimbali na kuwakumbusha Watanzania kuwa ni wakati wa
kumwabudu Mwenyezi Mungu.
Mkapa alisema mara nyingi alishauriana na viongozi
wa dini katika masuala ya kijamii na kiroho na kumtaja askofu mpya wa
Bukoba, Rwoma na Mtangulizi wake aliyestaafu Nestory Timanywa kuwa
alishirikiana nao katika masuala ya wananchi. Onyo la Mkapa limekuja
siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kukemea mambo ya kidini na
kutetea Serikali yake haiongozi kwa misingi ya ubaguzi.
Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, Rais
Kikwete alikwenda mbali zaidi na kudai amekuwa akilalamikiwa na viongozi
wa madhehebu ya Kikristo na yale ya Kiislamu.
Maneno ya Mkapa na Kikwete yamekuwa katika kipindi
hiki taifa likiwa limetikiswa na matukio yenye mwelekeo wa chuki za
kidini. Matukio makubwa yakiwa yale ya kuuawa wa Padri Evarist Mushi
huko Zanzibar na Mchungaji Mathayo Kachila wa Geita.
Pia kupigwa risasi kwa Padre Ambrose Mkenda na
kumwagiwa tindikali kwa Sheikh Fadhil Soraga na vurugu za mambo ya
kuchinja huko Geita na Tunduma.
Askofu Mpya wa Bukoba Rwoma alimshukuru Mkapa kwa
kuzungumzia umuhimu wa amani ya nchi, huku akisisitiza suala la upendo
miongoni mwa wananchi.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye jana alitaja
vyanzo vya vurugu zinazoendelea nchini kuwa unatokana na tofauti kubwa
kati ya walionacho na wasionacho.
Alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua santuri ya
nyimbo za dini kwa Kwaya ya Mt Joseph, Mfanyakazi ya Chuo Kikuu cha
Dodoma (UDOM).
Sumaye alionya kuwa kama hali ya
utajiri kwa baadhi ya watu itaachwa na kuendelea hivyo, ni wazi kuwa
nchi haitatawalika kwa amani.
“Binadamu mwenye njaa na aliyekata tamaa kamwe
hawezi kutawalika kwani kila wakati anahisi kutengwa na kundi jingine,”
alisisitiza Sumaye.
No comments:
Post a Comment