Dar es Salaam. Wakati Bunge la 11 la Bajeti
kwa mwaka huu likianza kesho, Kamati Kuu ya Chadema imesema itatumia
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kulibana Bunge kuhusu utendaji usiofuata
Kanuni za Bunge unaofanywa na Spika na wasaidizi wake.
Pia wabunge hao wameitaka Serikali kuweka wazi
mikataba iliyoingia hivi karibuni na Serikali ya China ili wananchi
waweze kufahamu kilichomo vinginevyo watatumia kambi hiyo kuwabana
wahusika.
Katika kikao cha 10 kilichomalizika Februari 8,
mwaka huu mjini Dodoma, Mnadhimu wa kambi hiyo, Tundu Lissu alisema kuwa
wanaandaa hoja za kumng’oa Spika na Naibu wake, Job Ndugai kwa kile
walichodai kukiuka kanuni mbalimbali za Bunge.
Kambi ya upinzani ilikuwa ikilalamika kuondolewa
kwa hoja binafsi za baadhi ya wabunge wao ikiwemo ya Mbunge wa Ubungo,
John Mnyika (Maji), James Mbatia (Mitalaa ya Elimu) na Joshua Nassari,
ambaye hoja yake ilihusu utendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa
(NECTA).
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda wakati
akiahirisha kikao cha 10, alisema kuwa hoja binafsi zitakuja tena katika
kikao cha 11 na wenye hoja watazifufua.
Jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa
Chadema, John Mnyika alisema Kamati Kuu ilibaini kwamba matukio
yaliyotokea katika kikao 10 yalitokana na meza ya spika kutofuata
kanuni.
“Tumeamua kwamba Kambi ya Upinzani Bungeni
itashughulikia tatizo hili la upindishwaji wa kanuni za Bunge ili
wahusika wabanwe kwa vitendo wanavyovifanya,” alisema.
Alisema kambi hiyo itafanya hivyo kwa kufuata
sheria na miongozo ambayo inawabana watendaji hao wa Bunge ili waweze
kuwajibishwa kwa vitendo vyao.
Akizungumzia mikataba, Mnyika alisema kamati hiyo
ina wasiwasi kuhusu mikataba 17 iliyoingiwa na Serikali za Tanzania na
China na kutaka iwekwe hadharani.
Baadhi ya mikataba iliyotiwa saini ni katika
kilimo, sekta ya afya, miundombinu ikiwamo mkataba wa ujenzi wa Bandari
ya Bagamoyo mkoani Pwani, ujenzi wa Reli ya Kati na ya Mamlaka ya Reli
ya Tanzania na Zambia (Tazara), kwenda maeneo mbalimbali nchini hali
itakayorahisisha usafirishaji wa mizigo.
Mikataba mingine ni uboreshaji wa sekta ya
viwanda, kilimo hasa cha tumbaku na kulipatia Shirika la Utangazaji
Tanzania zana za kufanyia kazi.
“Kamati Kuu inaitaka Serikali kuweka wazi
mikataba hiyo vinginevyo watataka ufafanuzi katika kikao cha Bunge la
Bajeti kinachotarajia kuanza rasmi kesho.
Kuporomoka kwa maghorofa
Mnyika alisema jopo la wanasheria wa chama hicho,
wanafanya uchunguzi wa kuangalia maghorofa yaliyowahi kuanguka na hatua
zilizowahi kuchukuliwa.
Alisema ingawa kuna watu ambao wamekuwa
wakifikishwa mahakamani, lakini vigogo wengi wamekuwa hawawajibishwi kwa
matukio yanayotokea.
“Tukikamilisha uchunguzi huo, tutalitumia
Bunge kuwabana wahusika ili wawajibishwe kwa vitendo vyao vya kushindwa
kusimamia sheria za ujenzi na kusababisha maafa,” alisema.
Kuteswa kwa Kibanda
Kamati hiyo imesikitishwa na kutekwa na kujeruhiwa
kwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari, Absalom Kibanda na huku
polisi wakiwa hawachukui hatua zinazotakiwa.
Alisema tukio hilo linafanana na lile la kutekwa
na kuteswa kwa kiongozi wa madaktari, Dk Steven Ulimboka na mauaji ya
Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi.
Mnyika alisema uchunguzi wa matukio hayo
unatia mashaka na kwamba kumekuwa na usiri katika uchunguzi unaofanywa
na polisi na hivyo Kamati Kuu inataka kuingilia kati ili kubaini ukweli.
Ufisadi bandari
Mnyika alisema katika Bunge lijalo watawasilisha
vielelezo bungeni vinavyoonyesha namna Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe alivyotoa zabuni ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kwa
Kampuni ya Jitegemee Trading Company Ltd inayodaiwa kuwa ya CCM, kinyume
na taratibu.
Madiwani wa Chadema
Mnyika alisema kumekuwa na madiwani wengi ambao wanakamatwa na polisi kwa makosa ambayo hayaeleweki.
No comments:
Post a Comment