Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo
Mpoki Bukuku, Mwananchi
Serikali imesema
itarudisha adhabu ya viboko kwa wanafunzi shuleni ili kujenga nidhamu na
kujituma.Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akizindua tovuti ya
www.shledirect.co.tz inayowezesha wanafunzi kujisomea kwa njia ya
mtandao, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo
ilisema kuondolewa kwa adhabu ya viboko shuleni kumewafanya wanafunzi
wengi kukosa nidhamu na wakati mwingine kujifanyia mambo kienyeji.
“Wasipotandikwa mambo hayaendi, nilipokuwa
mwalimu mkuu nilikuwa nawatandika kweli ndiyo maana shule yangu ilikuwa
ikiongoza Mkoa wa Mbeya hivihivi hawaendi...” alisema huku akishangiliwa
na wageni waalikwa.
Alisema watoto wa siku hizi wamekuwa wakitumia
vibaya teknolojia ambayo ingeweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa katika
masomo yao... “Tovuti kama hiyo ingewasaidia kwa masomo, lakini wao
wanakimbilia kwenye facebook na mambo mengine yasiyofaa.”
Aliyalaumu mashirika yasiyo ya kiserikali na
haki za binadamu ambayo yamekuwa yakipigania kuondolewa kwa adhabu hiyo
shuleni na kusababisha kushuka kwa nidhamu kwa kiasi kikubwa.
Kadhalika alisema Serikali imepiga marufuku
matumizi ya simu za mikononi kwa sababu baadhi ya wanafunzi wamekuwa
wakizitumia vibaya jambo ambalo linawarudisha nyuma kimasomo.
“Simu tunazipiga marufuku, mwalimu akimkuta mwanafunzi na simu amnyang’anye ndizo zinatuharibia taifa letu.”
Aliwapongeza wabunifu wa mtandao huo akisema ni wazalendo kwani wamekuwa msaada katika jitihada za Serikali kukuza elimu nchini.
“Watu wanapiga kelele Mulugo na Kawambwa
wajiuzulu, hata tukijiuzulu haitasaidia, bali kila Mtanzania atoe
mchango wake katika elimu ili kuweza kuiendeleza.”
Mwanzilishi wa
tovuti hiyo, Faraja Nyalandu alisema itakuwa na manufaa kwa wanafunzi wa
Tanzania kwani masomo yanayotolewa yanaandaliwa na walimu wazoefu wenye
shahada hivyo wanafunzi watakapoitumia watapata manufaa makubwa.
Maoni ya wadau
Akizungumzia
hatua hiyo ya Serikali, Waziri Kivuli wa Elimu Mafunzo ya Ufundi, Suzan
Lyimo aliitaka iache kuangalia mambo madogo ambayo yanachangia kwa
kiasi kidogo tu kudorora kwa elimu na kuacha mambo makubwa.
“Kuna mambo makubwa zaidi yaliyotufikisha hapa
tulipo, hii ni sawa na kushughulika na matawi na kuacha mizizi. Lazima
tuangalie suala hili kwa upana zaidi, kuna ripoti nyingi na nzito
hazijafanyiwa kazi mpaka sasa badala yake Serikali inaibuka na kuanza
kutangaza vitu vidogo kama hivyo, wafanyie kazi kwanza ripoti ambazo
zilitumia pesa nyingi za walipakodi kwani nyingi zina mapendekezo
mazuri.”
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mpwapwa, Rukonge Mwero alisema uzuri wa adhabu ya viboko ni kwamba haipotezi muda”
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo Bisimba alisema adhabu ya viboko haina
maana katika kipindi hiki akisema wanafunzi wanapaswa kupewa adhabu
ambazo zinawafundisha kama zile za kufanya usafi na kazi mbalimbali.
“Viboko havifundishi zaidi ya kumpatia
mwanafunzi maumivu na kusababisha aichukie shule. Waelimishwe kwa
kuelekezwa lakini wakiendelea kukiuka, wapewe adhabu za kufanya kazi
mbalimbali.
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT),
Gratian Mukoba alisema walimu hawapati faida yoyote kuwachapa au
kutowachapa viboko wanafunzi.
“Hawa viongozi kila kukicha wanazungumza mambo yasiyo na maana, badala
ya kuzungumzia masilahi ya walimu wanazungumza kuhusu viboko, hatuelewi
wakiamka kesho watasema nini,” alisema Mukoba.
No comments:
Post a Comment