Tunduma. Vurugu kubwa zilizuka jana katika Mji
wa Tunduma ambao ni makao makuu ya Wilaya ya Momba, Mkoa wa Mbeya, baada
kutokea mvutano mkali kuhusu nani anayepaswa kuchinja mifugo baina ya
waumini wa dini mbili; Waislamu na Wakristo.
Mamia ya polisi kutoka wilaya zinazouzunguka
Mji wa Tunduma walimwagwa na walilazimika kutumia mabomu ya machozi na
maji ya kuwasha ili kuwatawanya waandamanaji pia, kutuliza vurugu
zilizodumu kwa zaidi ya saa nne.
Vurugu hizo ambazo zinahatarisha amani,
zimetokea siku tatu tu tangu Rais Jakaya Kikwete aonye kwamba kwamba
vurugu zenye sura ya kidini ni hatari na zinaweza kuvuruga amani na
utulivu uliodumu kwa miaka mingi nchini.
Mijadala kuhusu vurugu hizo ilitawala katika
mitandao ya kijamii ikiwamo facebook, Mabadiliko Forum na Jamii Forums
ambako watu mbalimbali walionyesha kukerwa nazo, huku wakiitaka Serikali
ichukue hatua za kudhibiti.
Kutokana na vurugu hizo zilizoanza saa 4:30
asubuhi, wakazi wa mji huo walijifungia ndani kwa kuhofia usalama wa
maisha yao, huku maduka na shughuli za biashara nazo zikifungwa.
Mwandishi
wa Mwananchi aliyekuwa katika eneo la tukio anaripoti kwamba katika
vurugu hizo, watu zaidi ya 35 wamekamatwa wakiwamo Diwani wa Kata ya
Tunduma Frank Mwakajoka na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Gidion Mwamafupa.
Habari zaidi zinasema barabara za mji huo
zilifungwa, umeme ulizimika baada ya moto kulipuka kwenye moja ya nguzo
za umeme. Pia mpaka wa Tanzania na Zambia ulifungwa kwa muda.
Magari ya abiria na yale ya usafirishaji
yaliyokuwa yakitoka na kuelekea Zambia, Dar es Salaam, Sumbawanga na
Mbeya Mjini pia yalikwama na kusababisha usumbufu mkubwa kwa abiria.
Msikiti ulivunjwa na watu wawili akiwamo askari polisi walijeruhiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani
Athuman alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kwamba tukio hilo
limetokea wakati Serikali ikiwa kwenye mazungumzo na baadhi ya wahusika
katika mgogoro wakiwamo viongozi wa dini na wachinjaji wa nyama.
“Mgogoro wa kuchinja umedumu kwa siku tatu,
jana kamati ya ulinzi na usalama chini ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas
Kandoro ilikutana na baadhi ya viongozi wa dini na wadau wa kuchinja
nyama na kuna mambo matatu ambayo yalitolewa katika mkutano huo,”
alisema Diwani.
Alisema katika mkutano huo Kandoro aliagiza
kuwa wananchi wanatakiwa kuwa wavumilivu katika kipindi hiki, ambacho
Serikali ngazi ya kitaifa inalishughulikia na kuwataka kuendelea na hali
uchinjaji kama ilivyokuwa awali na kila mmoja afanye kile anachoamini
katika dini yake wakati wa kula.
Hata hivyo, baadhi ya Wakristo waliafikia
lakini wengine hawakuafiki. Hivyo jana asubuhi walihamasisha maandamano
katika mji huo ambayo yalisababisha vurugu hizo.
“Pamoja na hayo yote uchunguzi wa kitaalamu
tumebaini kuwa vurugu hizo siyo za kidini, bali zimehusishwa siasa kwani
hata viongozi wa dini waliohusika ni baadhi siyo wote ambao
wanajishughulisha na suala hili,” alisema Diwani.
Alisema kwa upande mwingine vurugu hizo zinafanywa na baadhi ya vijana wenye nia ya kuzitumia kwa lengo la kufanya uporaji.
No comments:
Post a Comment