Kile kilichodhaniwa kuwa kilele cha
sikukuu ya pasaka, kimegeuka msiba baada ya wachimba kokoto 20 kufukiwa
katika kifusi Jijini Arusha.
Hiyo ilikuwa ni kama ndimu katika kidonda kibichi,
kwani ni ijumaa iliyopita tu wakati watu wakijiandaa kwa sikukuu ya
Pasaka jengo la ghorofa 16 lilidondoka Jijini Dar es Salaam na kuua watu
36.
Vifo hivi vilivyotokea katika msimu wa sikukuu vimeweka idadi ya watu waliopoteza maisha kufikia 56 hivi, ndani ya siku nne tu.
Watu waliofukiwa na kifusi mkoani Arusha, walikuwa wakichimba kokoto katika eneo la Moshono.
Imeelezwa kuwa ni maiti 14 tu ndizo zilizoopolewa na watu wengine bado wanahofiwa kuwa ndani ya kifusi hicho.
Ilikuwa ni saa tano asubuhi, juzi, gema la kokoto
liliporomoka kisha kuwafunika wote waliokuwamo ndani, sababu kubwa
ikielezwa kuwa ni mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha mjini Arusha.
Vilevile magari mawili yaliyokuwa yamepaki pembeni kwa ajili ya kubeba mzigo huo yalizama ndani ya shimo hilo kubwa la kokoto.
Watu saba walikufa 1997
Inaelezwa kuwa hii ni mara ya pili kwa mgodi huu
kuua watu kwani mwaka 1997 wachimbaji wa kokoto walifukiwa na saba kati
yao walipoteza maisha.
Tukio la Dar
Mlinzi wa msikiti wa Shia, aliyeshuhudia kudondoka
kwa ghorofa hilo amesema alianza kuona mashine ya zege ikianguka
kutoka ghorofa ya 17 ambapo ujenzi wa sakafu ya ghorofa hiyo ulikuwa
ukiendelea.
Mlinzi huyo, Athuman Salum Mnere anasema alisikia
sauti ya kukatika kwa kitu, ghafla sauti kubwa ya maporomoko, kisha
mashine ya zege na baada ya sekunde kadhaa, jengo lote likawa chini.
Anasema walionusurika walianza kuwaokoa watoto
waliokuwa wakicheza mpira katika uwanja wa ndani ya msikiti uliokaribu
na jengo hilo.
Aliwakanya watoto waliopoteza maisha
Anasema aliwaambia watoto waliokuwa wakicheza mpira katika uwanja huo waende nyumbani lakini hawakusikia.
Hata kabla ya dakika tano kwisha, jengo hilo liliporomoka na wale wanne waliokuwa wamekaa katika benchi walifunikwa na jengo.
“Wengine waliumia vibaya, ndiyo hao walioko hospitali. Wale waliokuwa kwenye benchi walikufa palepale”anasema.
Shughuli za uokoaji zilimalizika juzi na eneo lilipokuwepo ghorofa hilo kubaki mithili ya shimo.
No comments:
Post a Comment