Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph Mbilinyi.
Dodoma. Mjadala wa Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo jana uliingia
dosari na kulazimika kusitishwa kwa muda baada ya Bunge kukubaliana na
hoja ya Mbunge wa Mbozi Magharibi (CCM), Godfrey Zambi kuwa Hotuba ya
Kambi ya Upinzani, imejaa uchochezi.
Zambi alitoa hoja hiyo wakati Mbunge wa Mbeya
Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi alipokuwa akiwasilisha hotuba ya Kambi
ya Upinzani kuhusu makadirio hayo, baada ya kuomba mwongozo wa Spika.
“Kuhusu utaratibu,” alisema Zambi. Baada ya
kurudia kauli hiyo mara kadhaa, Spika wa Bunge, Anne Makinda alimsitisha
Mbilinyi kuendelea na hotuba yake na kumpa Zambi nafasi.
“Mheshimiwa Spika, hotuba hii ya upinzani ni ya
uchochezi. Sisi kama Bunge hatuwezi kuruhusu ikaendelea kusomwa hapa na
Watanzania wakasikiliza uongo. Kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa 14,
imejaa uongo tu,” alisema Zambi na kuongeza:
“Kusema kwamba Tanzania inawatesa waandishi wa
habari kwa kuwang’oa meno na kucha, siyo kweli. Huu ni uchochezi na
ningependa kutoa hoja hotuba hiyo iondolewe bungeni, ni ya kichochezi.”
Baada ya kutoa hoja hiyo, karibu wabunge wote wa
CCM walisimama kumuunga mkono na baadaye, Spika wa Bunge Anne Makinda
alisimama na kusema: “Naomba wote mkae chini... kwanza kaeni,” kisha
aliendelea: “Humu humu bungeni, sisi wenyewe, tulipitisha kanuni kwamba
tusiingize neno uchochezi kwenye mijadala yetu. Haya, sasa naahirisha
kikao mpaka jioni na naagiza Kamati ya Kanuni iende ikapitie hotuba hiyo
kwanza kabla haijaletwa tena bungeni.”
Nje ya Bunge
Wakiwa wanatoka bungeni, mvutano ulioanzia ndani
ya ukumbi, uliibuka nje ya lango kuu la Bunge ambako wabunge kadhaa wa
CCM na Chadema waliendeleza mjadala huo na kuzozana hadharani.
Wabunge waliozozana kuhusu hotuba hiyo nje ya
ukumbi ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu, Mbunge wa
Same Mashariki (CCM), Anna Kilango, Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail
Aden Rage na Lucy Kihwelu (Viti Maalumu Chadema).
“Hamuwezi mkaharibu kanuni za Bunge letu kwa hotuba zenu za uchochezi,” alisema Kilango akimwambia Lissu.
“Hiyo kanuni ni ipi ambayo tumeiharibu? Huo ni ukorofi wenu tu, tunafahamu siku nyingi,” alijibu Lissu.
Baadaye akadakia Rage; “Hawa dawa yao ni .....”
Kauli hiyo ya Rage ilijibiwa na Kihwelu aliyemwambia “Makofi yako ni
Yanga tu. Umesahau umepigwa mabao 2-0.”
Mbilinyi atetea hotuba yake
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ukumbi
wa Bunge, Mbilinyi alitetea hotuba yake akisema kuwa haina tatizo lolote
na imefuata kanuni zote za kusomwa bungeni.
“Hili kwetu (Chadema) ni changamoto, ila niseme tu
kwamba hotuba yangu haikuwa na tatizo lolote na ilipitia hatua zote
halali kabla ya kusomwa bungeni,” alisema.
Utaratibu uliowekwa na Bunge unataka hotuba za hoja za bajeti kuwasilishwa kwa Spika siku mbili kabla ya kusomwa.
Alisema hotuba hiyo haina chembe ya uongo, akisema
ni ukweli kwamba waandishi nchini hawana uhuru wa kufanya kazi na
baadhi wanateswa na kunyanyaswa.
Baadaye jioni
Katika kikao cha jioni, Spika Makinda alitoa
mwongozo wake na kueleza sababu za kuahirisha hotuba ya Mbilinyi na
kusema anakubaliana na hoja iliyokuwa imetolewa asubuhi na Zambi kwamba
maneno yaliyopo katika hotuba ya Mbilinyi kuanzia ukurasa wa kwanza hadi
wa 14 yaondolewe kwa kuwa yanaingilia Mahakama.
“Kwa kutumia Kanuni ya 72 ni mamlaka ya Spika
kusimamia Bunge hivyo kwa kutumia Kanuni ya 64, naagiza maneno yote
yanayozungumzia mauaji ya Daudi Mwangosi yaondolewe,” alisema Spika
Makinda.
Alisema amefikia uamuzi huo baada ya Kamati ya
Kanuni kupitia hotuba hiyo na kuona kwamba maneno yaliyopo katika kurasa
hizo yanaingilia mhimili wa mahakama.
Baada ya Spika kueleza hayo, Mbilinyi aliruhusiwa
kuendelea na hotuba yake na kuomba kuanzia jana jina la Sugu lisitumike
tena bungeni.
No comments:
Post a Comment