Majeruhi wa mlipuko wa bomu Arusha, Mwalimu Fatuma Tarimo akionyesha
kipande cha chuma baada ya kuondolewa kwenye mguu wake, katika
Hospitali ya Muhimbili Dar es Salaam jana.
Dar es Salaam/Arusha. Bomu
lililorushwa na kuua watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 60 kwenye
Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi huko Arusha, inadaiwa
lilitengenezwa kienyeji.
Wakati kukiwa na madai hayo, mazishi ya marehemu
hao Regina Kurusei, (45), James Gabriel (16) na Patricia Joachim (9)
yanatazamiwa kufanyika leo Olasiti, Arusha na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
anatarajiwa kuhudhuria.
Ofisa mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alimdokeza
mwandishi wetu jana kuwa kwa ujuzi na uzoefu wake wa masuala hayo, bomu
hilo si la kiwandani akisema msingi wa imani yake ni jinsi vyuma
vilivyotawanyika na kuumiza watu zaidi ya 20.
Watu saba wamefikishwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kuondolewa vyuma na kupata matibabu zaidi.
Mstaafu huyo alieleza kuwa mabomu mengi zaidi ya
kienyeji hutengenezwa kwa kutumia bakuli za chuma, zikiwekewa baruti
ndani na kufungwa kwa waya.
“Hawa jamaa huweka vipande kama 36 vya baruti na
hufungiwa ndani ya bakuli kwa kubanwa sana ili kuvipa joto na bomu
likitua, husababisha madhara makubwa,” alisema ofisa huyo ambaye
alishiriki Vita ya Uganda mwaka 1978 hadi 1979.
Mstaafu huyo alisema mabomu ya aina hiyo
yametumika kwenye mashambulizi ya kigaidi katika nchi mbalimbali duniani
kama Lebanon, Vietnam, Libya, Ireland Kaskazini, Syria, Afghanistan,
Iraq, Chechnya na India.
Mmoja wa majeruhi, Mwalimu Fatuma Tarimo amesimulia alivyoshuhudia bomu likitua mbele yake na kulipuka.
Tarimo, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili, alisema jana kuwa aliliona bomu hilo likiwa na rangi ya
shaba. Pia alisema lilikuwa na waya kwa juu.
“Baada ya kutua, nilisikia kishindo kikubwa
nikashtuka ikabidi niangalie. Baada ya kuona ni kitu kama chuma nilipata
hofu nikafikiria kuondoka,” alisema mwalimu huyo wa Shule ya Msingi ya
Burka Estate, nje kidogo ya Jiji la Arusha. Hata hivyo, alisema kabla ya
kuondoka, alishtukia amenyanyuliwa juu na hakujua kilichoendelea kwani
aliposhtuka alijikuta akiwa katika Hospitali ya Mount Meru.
Tarimo ametolewa kipande cha chuma katika mguu wake wa kulia.
“Nina
maumivu bado lakini nina matumaini nimechukuliwa kipimo cha ‘T-Scan’
kwa matibabu zaidi,” alisema Mwalimu Tarimo ambaye anaaminika kuwa na
kipande kingine kwenye mapafu.
Majeruhi mwingine, Jenipher Joackim ambaye amefiwa
na mwanaye Patricia Joackim (9) hana taarifa za kifo hicho kilichotokea
katika Hospitali ya KCMC.
“Nimeambiwa kwamba yupo ICU sijui anaendeleaje,” alisema.
Jeshi la Polisi mkoani Arusha limetangaza donge nono la Sh50 milioni kwa
watu watakaosaidia upelelezi wa ulipuaji bomu huku likiwashikilia na
kuwahoji watuhumiwa 12 hadi sasa.
No comments:
Post a Comment