Waziri Nchimbi awapasha wapinzani

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi 


Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi juzi aliwaondolea uvivu wapinzani na kuwaeleza kuwa hawezi kujiuzulu wala kufanya kazi kwa shinikizo la wanasiasa.

Mbali na hilo, aliwataka wapinzani kugombea na kupata nafasi za urais ili waweze kuweka utaratibu wa kuwafukuza mawaziri wao watakaoona hawafanyi kazi ipasavyo.

Nchimbi alitoa kauli hiyo wakati akijibu hoja kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka 2013/14.

“Nataka kumwambia ndugu yangu Lissu kuwa, kazi ya wagombea wote ni kuomba ridhaa ya kuchaguliwa ili waweze kuweka taratibu za kuajiri na kufukuza,hivyo ili kumwondoa waziri, nawashauri nanyi mgombee urais na mpate ili mjiweke katika nafasi ya kufukuzana,” alisema Nchimbi.

Alimsifia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda kuwa anafanya kazi nzuri licha ya malalamiko yanayotolea na wanasiasa na baadhi ya wanaharakati na kusema hatakiwa kuacha kazi hiyo kwa shinikizo hizo.

Hata hivyo alikubaliana na hoja iliyotolewa na msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Vicent Nyerere kuwa kuna silaha nyingi ambazo zimezagaa nchini.

“Hilo nakubaliana nalo, kuna ongezeko la silaha nyingi nchini jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa raia wetu,mbali na hilo pia nachukizwa na vitendo vya rushwa ndani ya jeshi la polisi”.

Alisema Serikali imejipanga vizuri kwa ajili ya kukabiliana na vitendo hivyo na kuwawajibisha askari wake ambao si waaminifu ndani ya jeshi.

No comments:

Post a Comment