Bandari
Dar es Salaam. Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) imetangaza rasmi kuanza kwa utaratibu wa kukagua
bidhaa zote zinazoingizwa nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam, ili
kuhakiki wingi, aina na kiwango cha kodi kinachotakiwa kulipwa.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Serikali lililotolewa bungeni, June 6 mwaka huu na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.
Dk Mgimwa alitoa agizo hilo kufuatia kugundulika
kwa mbinu zilizokuwa zikitumiwa na baadhi ya wafanyabiashara, kutoa
taarifa za uongo kuhusu bidhaa wanazoingiza kwa lengo la kukwepa kodi.
Taarifa iliyotolewa jana na Kamishna wa Forodha na
Ushuru wa Bidhaa, Tiagi Masamaki ilisema bidhaa zilizokuwa zikiondolewa
bandarini bila ukaguzi, sasa zitakaguliwa na ikionekana kuna na taarifa
zisizo sahihi hatua za kisheria zitachukuliwa.
“TRA itamchukulia hatua za kisheria mwagizaji au
wakala atakayebainika kutoa taarifa za uongo, hatua hizo ni kutaifisha
mali, kufuta leseni ya uwakala wa forodha na kushtakiwa,” alisema
Masamaki.
Alisema waagizaji wa bidhaa na mawakala wa forodha
wanatakiwa kutoa taarifa sahihi kwa TRA kuhusu bidhaa walizoziagiza,
kulipa kodi stahiki kabla ya kufanya ukaguzi ili kukwepa usumbufu.
Alisema ukaguzi hautazihusisha bidhaa
zinazoingizwa nchini kama malighafi za viwandani, bidhaa kwa ajili ya
miradi inayogharimiwa na wahisani na mali za balozi mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment