Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
Dodoma. Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepinga
muundo wa Muungano wa Serikali tatu unaopendekezwa katika rasimu ya
Katiba Mpya iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba mwanzoni mwa
wiki iliyopita.
Chama hicho tawala kimesema bado kinaamini katika muundo wa Serikali mbili.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kwamba mapendekezo
yaliyowasilishwa mbele ya Tume hiyo yanabaki kama yalivyo, hivyo msimamo
wao ni kuwapo kwa muungano wenye muundo wa Serikali mbili.
“Mapendekezo ambayo ndiyo msimamo wa chama
tulishayawasilisha kwenye Tume kuwa sisi tunapendekeza mfumo wa Serikali
mbili na siyo tatu wala moja,” alisema Nape alipokuwa akitoa taarifa ya
uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ya CCM iliyokutana usiku wa kuamkia jana
kujadili suala hilo.
Kauli ya Nape inafanana na matamshi ambayo
yamewahi kutolewa na baadhi ya wanasiasa wakongwe ambao ni makada wa CCM
wakiwamo, mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na John Malecela,
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na baadhi ya
wabunge ambao mara kadhaa wamekaririwa wakipinga pendekezo la Serikali
tatu.
Hata hivyo, Nape alisema matamshi ya viongozi hao
yalikuwa ni maoni yao binafsi na kauli yake ndiyo rasmi ya chama
hicho... “Mimi ndiye msemaji wa chama hiki. Ndiye ninayeeleza msimamo wa
chama chetu, yanayozungumzwa na watu wengine hata kama ni viongozi siyo
msimamo wa chama ni maoni yao binafsi.”
Habari ambazo gazeti hili ilizipata zinasema
katika kikao hicho cha CC kulijitokeza hofu ya suala la wananchi kuwa na
mamlaka ya kuwang’oa wabunge ikiwa hawatatekeleza masilahi yao na
kwamba pendekezo hilo lina upungufu kwani halitafsiri masilahi hayo ni
yapi.
Waunda kamati
Nape alisema rasimu iliyotolewa na Tume siyo
waraka wa mwisho kwani bado unatoa fursa kwa Watanzania kuijadili na
kutoa maoni yao na kwamba CCM kitatumia nafasi hiyo kuwasilisha maoni
yake kuhusu jambo hilo.
Alisema chama hicho kitawasiliana na wanachama wake zaidi ya 6,000 nchini ili waendelee kutoa maoni yao kuhusu suala hilo.
“Wengi wanadhani rasimu hii ndiyo ya mwisho… hii
ni ya mwanzo tu, itajadiliwa italetwa ya pili na ya tatu, kwa hiyo
hatuwezi kusema kilichoelezwa kwenye tume ndiyo msimamo. Ndiyo maana
tumeamua kurejesha suala hili kwa wanachama wetu liendelee kujadiliwa,”
alisema na kuongeza:
“Kama wanachama wetu wakiamua kuwepo kwa Serikali
tatu, hatutachakachua, tutayachukua na kuyapeleka kama msimamo wetu,
lakini tutakubaliana ikiwa uamuzi utakuwa umewahusisha wanachama wetu
katika ngazi zote.”
“Hatuangalii kipengele kimoja tu. Tutapitia vipengele vyote hadi
kuzimaliza kurasa zote zaidi ya 70 zinazoainisha mapendekezo ya Tume ya
Jaji (Joseph) Warioba.”
Alisema wanachama wake wanapaswa kuipitia na
kuijadili rasimu hiyo kwa kuzingatia mapendekezo kilichoyatoa awali
wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya.
“Tulitoa maoni yetu na sasa tunaijadili Rasimu ya
Katiba Mpya kwa kuzingatia maoni yetu yale, CCM tunakwenda kwa mujibu wa
sheria,” alisema. Habari kutoka ndani ya CC ya CCM zinasema chama hicho
kimeipa kazi kamati ambayo ilitumika kuandaa mapendekezo yake awali,
kupitia rasimu hiyo na kufanya ulinganisho wa yale ambayo chama hicho
kilipendekeza dhidi ya yale yaliyozingatiwa katika Rasimu ya Katiba
hiyo.
“Kamati itafanya ulinganisho na baada ya hapo
tutakwenda kwa wanachama kuwaeleza ni yapi tulipendekeza kama chama na
ni yapi ambayo Tume imeyazingatia na hapo tutapata mawazo yao ambayo
tutayatumia katika ngazi ya mabaraza ya Katiba,” kilisema chanzo chetu.
No comments:
Post a Comment