Wasanii waelimishwe athari za ulevi


Mwishoni wa wiki iliyopita nilikutana na msanii wa Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ Msafiri Diouf kwenye Viwanja wa Leaders Club, Dar es Salaam.

Alinimbia: “Nimeacha kutumia dawa za kulevya, si unaniona hata afya imerudi? Mimi siyo tena mtumiaji wa unga kwa miezi tisa sasa. Naomba Mungu anisaidie nisirudi nilipotoka.”

“Kuna wasanii wengi wanatumia madawa ya kulevya, wasipokata shauri na kubadili tabia kama mimi watapukutika na kuisha kabisa. Binafsi niko tayari kumsaidia atakayehitaji msaada wangu.”

Kikubwa ambacho ningependa kukizungumzia hapa ni kiasi gani wasanii wetu, vijana wanapuputika ama kupoteza mwelekeo wa maisha kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Tatizo hili siyo tu kwa Tanzania, bali kaya yote ya dunia hasa vijana wa fani mbalimbali. Filamu, muziki, urembo, michezo wote ni waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya.

Msanii wa Uingereza Amy Winehouse, malkia wa muziki wa Pop, RnB na Soul wa Marekani, Whitney Elizabeth Houston na Brenda Fassie wa Afrika Kusini, ni miongoni mwa wasanii walipoteza maisha kwa kuhusishwa na dawa za kulevya.

Tathmini za karibuni zinaonyesha kuwa, matumizi ya dawa za kulevya kwa wasanii inazidi kuongezeka na hivyo kutishia kizazi cha sasa kuharibika kwa kiasi kikubwa.

Kuna baadhi ya wasanii ambao matumizi ya dawa za kulevya yaliwaletea matatizo na kujikuta wakifikishwa katika hospitali ya wagonjwa wa akili, Mirembe iliyopo Dodoma kwa ajili ya matibabu zaidi, na wengi wao wamedai kujitumbukiza katika utumiaji huo wa dawa za kulevya kunatokana na baadhi ya watu waliochangia kuwarudisha chini kimuziki.

Nathubutu kusema wasanii wetu ambao wengi wao wamekuwa wakichukulia maisha ni leo na hawaangalia baadaye, sitaki kuwataja lakini tumeshuhudia wengi wakipata mafanikio makubwa katika kazi zao na kutumia pesa nyingi katika anasa.

Kama kila anayeshuka katika maisha akatumia dawa ya kulevya tukaona alistahili kufanya hivyo, kweli tutajenga taifa gani la kesho? Wangapi wana matatizo wanaangalia njia bora ya kuyatatua na hawatumii dawa za kulevya.

Nafahamu yapo mengi ambayo hupelekea kubomoa mwelekeo wa maisha ya binadamu hasa vijana, ambao ndiyo nguvu kazi ya maisha yao binafsi, familia zao na taifa kwa jumla.

Uvutaji wa bangi, kunywa pombe kupita kiasi, matumizi ya mirungi na dawa za kulevya ni baadhi ya starehe ambazo vijana wengi hasa wenye vipato vya wastani wamekuwa wakijihusisha navyo.

 

Kila kukicha ongezeko la utumiaji wa vilevi limekuwa likiongezeka na kuzidi kupunguza nguvu kazi, bila ya watumiaji kufahamu kwa bahati mbaya au makusudi kuhusu madhara ya utumiaji wa vilevi hivi.

Tumeiona mifano mingi na bado kasi inaongezeka kama vile watu hawaelewi athari za dawa za kulevya, mfano wa karibuni wa wazi ni msanii Ray C ambaye kama siyo msaada wa watu akiwamo Rais Jakaya Kikwete basi bila shaka angekuwa miongoni mwa waathirika wakubwa.

Nionavyo mimi, wasanii wajue dawa za kulevya siyo suluhisho la matatizo yao wakati wa shida na badala yake watumie muda wao kufikiria jinsi ya kudumu katika soko la ushindani.

Ni changamoto kubwa pia kwa Serikali yetu ambayo imeshindwa kuweka sera ya kueleweka ya kulinda masilahi ya wasanii kiasi cha kazi za wasanii kuibwa kirahisi na wajanja.

No comments:

Post a Comment