JK: Acheni urafiki wa dhambi na wachimbaji wakubwa

Rais Jakaya Kikwete 


Rais Jakaya Kikwete ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuacha urafiki wa dhambi na baadhi ya wachimbaji wakubwa wanaohodhi maeneo makubwa na badala yake wazingatie sheria ili kutoa haki kwa wachimbaji wadogo.

Akizungumza katika siku yake ya mwisho kutembelea Mgodi wa Dhahabu wa Baraka uliopo wilayani Geita katika Kijiji cha Nyaruyeye juzi, Rais Kikwete alisema kilio cha wachimbaji wadogo hivi sasa ni maeneo lakini wanaweza kuchimba sawa na wachimbaji wakubwa hivyo kuitaka wizara hiyo kuzingatia sheria kwa kuwafutia umiliki wenye maeneo ambayo hawayafanyii kazi.

“Mkiyatwaa watapiga kelele, acheni wapige kelele lakini timizeni sheria. Masele (akimwangalia Naibu Waziri Nishati na Madini Stephen Masele) na wenzako lazima mzingatie sheria. Wanyang’anyeni maeneo haya wapeni wachimbaji wadogo wachimbe. Acheni kufanya urafiki wa dhambi na hawa,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete ambaye alieleza kufurahishwa kwake na wachimbaji wadogo kuanza kuchimba kisasa alisema sheria ya umilikaji wa maeneo ya utafiti na uchimbaji wa madini inaelekeza kuwa iwapo mwombaji akija kuomba tena (renewal) leseni ya eneo alilopewa anapaswa kulipunguza kwa asilimia 50 ili wapewe wengine na vivyohivyo anapokuja kwa mara ya pili, pia anapaswa kupunguziwa eneo lake kwa asilimia 50.

“Pamoja na kwamba sheria ipo wazi, ukiwauliza wizara kwa nini hawafanyi hivyo, hawana maelezo wapo kimya, sijui wanaingia kigugumizi gani kutimiza sheria hii. Wanaposhindwa kufanya haya ni hasara kwa taifa maana haya madini hayachimbwi, wangezingatia sheria hii na kuchukua maeneo haya wangewapa wengine wakachimba leo tusingekuwa na kelele za wachimbaji wadogo,” alisema. Rais Kikwete alisema madini yakiwa chini hayana thamani yoyote mpaka yanapochimbwa na kubainisha kwamba iwapo watu waliopewa leseni watazishikilia bila ya kuendeleza maeneo yao, watakwamisha ajira na maendeleo kwa nchi.

Aidha, aliitaka wizara hiyo kuwa makini wakati wa kutimiza matakwa ya sheria hiyo ya umiliki wa maeneo ya uchimbaji, akitahadharisha kuwa wamiliki wengine wanaweza kubadili majina pindi watakaponyang’anywa maeneo yao.

“Wana tabia ya kubadili majina, mkimnyang’anya atakuja upya. Kama alikuwa anaitwa Kikwete & Sons sasa atakuja tena anajiita SK lakini ndiye huyohuyo, tazameni sana. Najua, mnayajua mengi maana na ninyi ni wabia wao lakini ninachotaka ni kuzingatia na kusimamia sheria,” alisema.

Akizungumzia Mgodi wa Mzawa alioutembelea, Rais Kikwete alisema amejionea jambo kubwa na la kushangaza kiasi cha kusema kwamba iwapo angeishia kusimuliwa mambo hayo na watu bila ya kufika, asingeamini kama Watanzania wanaweza kuendesha migodi kama huo.

Alisema Serikali inathamini mchango wao na kuwataka kujiandikisha Tume ya Uwekezaji ili nao waweze kuomba msamaha wa mafuta na zana mbalimbali kama ilivyo kwa wawekezaji wakubwa wa nje.

Awali, Masele alimwomba Rais kuangalia uwezekano wa kuwapatia wachimbaji wadogo msamaha wa kodi akisema vifaa wanavyotumia havina tofauti na vile vya wachimbaji wakubwa.

No comments:

Post a Comment